Waziri wa Nishati na Madini , Profesa Sospeter Muhongo (wa
kwanza kulia) , Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Marcel Escure (kulia kwa
Waziri), Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa Bw. Eric
Besson (kulia kwa Balozi), pamoja na mtendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa
nchini, wakifurahia jambo mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyolenga katika kuendeleza
sekta za Nishati na Madini nchini.
Na Teresia Mhagama
Balozi wa Ufaransa nchini Bw. Marcel Escure akiongozana na Waziri
mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa, Bw. Erick Besson
wamemtembelea wizarani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
ili kufahamu fursa za uwekezaji katika sekta za Nishati na Madini.
Waziri huyo mstaafu wa Ufaransa, Bw.Erick Besson alikuwa akiiwakilisha
kampuni ya GDF Suez ya Ufaransa.
Katika suala la usimamizi wa bomba la gesi asilia, Profesa Muhongo
alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) litahitaji
kupata uzoefu na pengine mbia aliyebobea katika usimamizi wa bomba hilo
atakayeshirikiana na TPDC katika usimamizi wa bomba la gesi nchini.
Kuhusu umeme, Waziri Muhongo alimweleza Waziri mstaafu huyo
wa Ufaransa kwamba serikali inajikita katika miradi ya usambazaji umeme kwa
utaratibu wa ubia au mikopo ya bei nafuu na ina mpango wa kujenga njia ya umeme
ya msongo wa 400kv kuelekea ziwa Tanganyika hivyo aliikaribisha kampuni ya GDF Suez
kuwekeza katika miradi hiyo ya usambazaji umeme.
Aidha Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Madini
la Taifa (STAMICO) linatafuta mbia watakayeshirikiana naye katika kuendesha
mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, Kiwira mkoani Mbeya hivyo
kama wana nia ya kuwekeza katika eneo hilo pia wanakaribishwa kuingia katika
ushindani wa kupata nafasi hiyo.
Naye Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa,
Bw. Besson alimshukuru Profesa Muhongo kwa taarifa nzuri kuhusu fursa za
uwekezaji nchini na ameahidi kupata taarifa zaidi za uwekezaji katika mashirika
ya TPDC, STAMICO na TANESCO ili kuona jinsi kampuni ya Suez itakavyoshirikiana
na mashirika hayo katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini.


Hakuna maoni :
Chapisha Maoni