.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 27 Julai 2014

BALOZI SEIF AWATAKA VIONGOZI NA WANACHAMA WA CCM KUENDELEZA MSHIKAMANO WAO


Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM la Mombasa Kwamchina Nd. Ahmada Abdullwakil akitoa maelezo ya ujenzi wa tawi hilo mbele ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi.

Balozi Seif akikabidhi mchango wa Shilingi Milioni 4,00,000/- Kwa Mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Kwamchina Bibi Subira Kahalani Uria kwa ajili ya ununuzi wa mbao zitakazotumika kuezekea Tawi hilo.

Mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Kwamchina Bibi Subira Kahalani Uria akionyesha fedha taslim shilingi Milioni 4,000,000/- zilizotolewa mchango na Mjumbe wa NEC Balozi Seif Ali Iddi aliyepo pembeni yake kwenye eneo la Tawi hilo liliopo Mtaa wa Mombasa Kwamchina.

                                                               Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Viongozi na Wanachama wa chama hicho hivi sasa wanapaswa kuongeza mshikamano na umoja walionao katika dhana nzima ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Alisema mshikamano huo ndio silaha pekee itakayokiwezesha chama hicho kuwa na nguvu za ziada za kushinda na kuendelea kuongoza Dola ndani ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo katika hafla fupi ya kukabidhi mchango wa shilingi Milioni Nne { 4,000,000/- } kwa ajili ya ununuzi wa mbao zitakazosaidia kuendeleza kazi ya uezekaji wa Tawi la CCM la Kwamchina liliopo ndani ya Wilaya ya Dimani Mkoa wa Magharibi Kichama.

Balozi Seif alieleza kwamba CCM ina kazi kubwa katika kujiandaa na uchaguzi Mkuu huo ambapo alifahamisha kuwa kama zipo hitilafu ndogo ndogo baina ya wanachama na Viongozi hao wakati wa kuzirekebisha ni sasa ili kujenga safu isiyo shaka wala mikwaruzo.

Balozi Seif ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa Tawi hilo la Kwamchina aliwapongeza wana CCM wa Tawi hilo kwa umahiri wao wa kujenga Ofisi yenye hadhi inayokubalika na chama.

Alisema Ofisi za Chama cha Mapinduzi zinazojengwa katika maeneo mbali mbali hapa nchini lazima zilingane na hadhi ya chama Tawala na kamwe haipendezi kuona baadhi yake haziko katika kiwango kinachokubalika kama kilivyo chama chenyewe.

“ Nia ya Chama cha Mapinduzi ni kuona Ofisi zake za Matawi, Majimbo pamoja na Maskani zinajengwa na kuimarishwa katika hadhi ya chama chenyewe Tawala “ Alisema Balozi Seif.

Akizungumzia suala la Bunge Maalum la Katiba linalotarajiwa kuendelea tena mapema mwezi ujao Mjini Dodoma Balozi Seif alisema mchakato wa majadiliano ya kupata katiba mpya utaendelea kama kawaida kwa wajumbe wa Bunge hilo.

Alifahamisha kwamba Taifa la Tanzania linapaswa kuwa na Katiba imara itakayoshirikisha kila mwananchi wa Jamuhuri ya Mungano ambapo wajumbe hao ndio waliobeba dhamana ya uwakilishi wa wananchi hao.

Balozi Seif alieleza kwamba ili kazi hiyo ya majadiliano ya mchakato wa kupata Katiba mpya ikamilike vyema kila mjumbe wa Bunge hilo anawajibika kujadili mapendekezo yaliyotolewa na Wananchi na kuweka pembeni utashi wake binafsi.

“ Itapendeza kuona mchakato mzima wa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania unamuhusisha kila Mtanzania yakiwemo makundi yote ya jamii kama vile akina mama,watoto pamoja na watu wenye ulemavu “. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM la Kwamchina ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Nd. Ahmada Abdulwakil alisema kazi za uezekaji wa Tawi hilo zinatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Nd. Ahmada alisema uezekaji huo utaenda kama ulivyopangwa kwa vile Mabati 236 yaliyotolewa mchango na Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif takriban miezi saba sasa iliyopita zipo tayari kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanachama na Viongozi wenzake wa Tawi hilo la CCM la Kwamchina Mzee wa Tawi hilo Othman Bakari amemsifu Balozi Seif kwa umadhubuti wake wa mfano katika kutekeleza ahadi anazotoa kwa wanachama na hata kwa wananchi katika sehemu mbali mbali hapa Nchini.

Mzee Othman Bakari alisema jamii imekuwa ikishuhudia kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Balozi Seif akiwa ni Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nafasi ya Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Ujenzi wa Tawi la CCM la Kwamchina umeanza mara tuu baada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani wa mwaka uliopita baada ya kukamilika kwa taratibu za maandalizi ya ujenzi wake.

Tawi la CCM la KwaMchina litakapokamilika kwake linatarajiwa kuwa na Ofisi za Jumuiya mbali mbali za Chama hicho, ukumbi wa mikutano pamoja na eneo la vitega uchumi vitakavyosaidia uwezeshaji wa huduma za Ofisi hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni