Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za
rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Dkt. Parseko V.
Ole Kone kuomboleza kifo cha aliyepata kuwa Naibu Waziri, Mbunge na
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mheshimiwa
Alhaji Mahami Rajab Kundya.
Mzee Kundya aliaga dunia jana,
Jumapili, Julai 27, 2014 mjini Zanzibar.
Katika salamu zake, Rais Kikwete
amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa taifa limempoteza Mzee
Kundya katika kipindi ambacho ushauri wake ulikuwa unahitajika sana
na kuwa Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa mchango wake katika
nafasi zote alizozishikilia za Serikali, za Chama cha Mapinduzi na za
kidini.
“Naungana nawe na wana-Singida
wote katika kuomboleza kifo cha Mzee Kundya.Tumepoteza kiongozi
ambaye mchango wake utaendelea kukumbukwa na sisi sote. Kupitia
kwako, natuma pia salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu.
Niko nao katika kuomboleza msiba huu
mkubwa na naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi
roho ya Marehemu Mzee Kundya,” amesema Rais Kikwete.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Julai,2014
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni