Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi leo amekizindua rasmi Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha wanawake kiliopo Mtaa wa Mwera { Mwera Fitness Club } ndani ya Wilaya ya Magharibi.
Uzinduzi huo ameufanya katika viwanja vya michezo vya Skuli ya Regeza Mwendo na kushirikisha vikundi kadhaa vya mazoezi vya hapa Unguja wakijumuika pamoja na Viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo chini ya Waziri wake Said Ali Mbarouk.
Balozi Seif Ali Iddi aliyaongoza maandamano ya wana vikundi mbali mbali katika uzindui huo yaliyoanzia Mtofaani kupita Kituo cha Polisi cha Muembe Mchomeke na kuishia katika Viwanja vya Skuli ya Regeza Mwendo.
Akizungumza na wanavikundi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema watu wengi wanaendelea kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa viungo kutokana na kuugua maradhi ambayo yanaweza kuondoka kabisa iwapo jamii itajipangia utaratibu wa kufanya mazoezi.
Balozi Seif alisema ongezeko la wananchi kukimbilia Hospitalini kupata huduma za afya sambamba na Serikali kuu kuagiza dawa zinazogharimu fedha nyingi litapunguwa endapo watu wengi watafanya mazoezi kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba wananchi kujipangia utaratibu wa kufanya mazoezi ya kila siku mara wamalizapo ibada yao ya sala ya alfajiri kabla ya kuanza harakati zao za Kimaisha.
“ Mazoezi hata wazee yanawafaa kwa sababu muda wote yanasaidia kuimarisha viwili wili na akili “. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba michezo inaleta urafiki baina ya vikundi na hata mtu na mtu ikiwa ni moja ya mafanikio makubwa katika kuimarisha nyanja za michezo na kuondosha maradhi mbali mbali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa juhudi zake za kuhamasisha vikundi tofauti nchini kushiriki katika mazoezi ya viungo.
Mapema Mwenyekiti wa zoni D ya Vikundi vya mazoezi Zanzibar Juma Khalid alisema Chama cha Vikundi vya Mazoezi Zanzibar { ZABESA } iliamua kuvigawa vikundi vya mazoezi Zanzibar kwa lengo la kupata ufanisi mzuri.
Juma Khalid alisema Vikundi vya mazoezi ya viungo lengo lake kuu ni kuhakikisha kwamba sekta ya afya Nchini inapunguza uagizaji wa dawa ambazo zina gharama kubwa kwa kuhamasisha watu kufanya mazoezi ya viungo.
Mwenyekiti huoyo wa Zoni D ya vikundi vya mazoezi ya viungo aliwataka viongozi wa ngazi mbali mbali nchini ziwe zile za taasisi ya uuma na hata binafsi wafanye mazoezi ili kuweka viwili viwili vyao katika hali ya afya.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema Wizara hiyo itaendelea kuhakikisha kwamba Jamii yote inashawishika katika kufanya mazoezi.
Waziri Mbarouk alieleza kwamba hatua hiyo mbali ya kutunza afya kupitia mazoezi lakini pia itamfanya kila mwana mazoezi kuwa makini wakati wote kiakili na kimwili katika harakati zake za kila siku.
Uzinduzi huo wa kikundi cha mazoezi cha Mwera Fitness Club uliambatana na mchango wa papo kwa papo kusaidia kuimarisha kikundi hicho kichanga kilichoanzishwa mwaka mmoja uliopita na kukifanya kuweka rikodi ya kufikia vikundi 60 vya mazoezi hapa Zanzibar.
Zaidi ya shilingi Milioni 3,000,000 zimechanga na kutolewa ahadi katika mchango huo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni