Jumatatu, 30 Machi 2015
MAALIM SEIF AUNGURUMA VIWANJA VYA JAMUHURI JIMBO LA MAKUNDUCHI, AWATAKA WANACHAMA WA CUF KUENDELEA KUENDESHA SIASA ZA KISTAARABU
Na: Hassan Hamad, OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewanasihi wanachama wa chama hicho kushikilia msimamo wao wa kuendesha siasa za kistaarabu na kuacha kufikiria kulipiza kisasi kufuatia hujuma zinazofanywa dhidi ya chama hicho.
Amesema lengo kubwa la hujuma hizo zikiwemo kuchomwa moto kwa ofisi za chama hicho ni kutaka kukitoa katika malengo yake ya kupigania haki za wananchi, na kwamba njama hizo hazitoweza kufanikiwa.
“Nakunasihini sana wanachama wa CUF musichokozeke, hawa wanaofanya hujuma hizi wana lengo la kututoa katika malengo yetu ya kupigania haki, lakini nakuombeni musiuingie mtego huo”, alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Jamhuri, jimbo la Makunduchi.
Amewashukuru wananchi wa Makunduchi kwa mwamko wao waliouonyesha katika kukiunga mkono chama hicho ambapo jumla ya wanachama wapya 584 wamejiunga na CUF kwenye mkutano huo, miongoni mwao wakiwemo makada wa Chama Cha Mapinduzi.
Amesema hatua hiyo inadhihirisha jinsi wanachama wa CUF katika maeneo mbali mbali nchini wanavyoweza kuungana kwa ajili ya kutetea haki zao bila ya kujali maeneo wanayotoka.
Akizungumzia mipango ya chama hicho, Maalim Seif amesema kinakusudia kuleta mabadiliko kwa kujenga uchumi imara ambapo kila mwananchi ataweza kunufaika na rasilimali zilizopo.
Zanzibar inazo rasilimali na fursa nyingi za kiuchumi lakini bado hazijatumika ipasavyo kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini, na kwamba endapo CUF kitashika hatamu za dola, kitaziibua fursa hizo na kupelekea vijana wengi kuweza kupata ajira katika sekta mbali mbali zikiwemo kilimo, uvuvi, biashara, utalii na viwanda vidogo vidogo.
Kuhusu katiba inayopendekezwa, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali bado haijawahi kukaa na kutoa msimamo juu ya katiba hiyo, na kufafanua kuwa hakuna msimamo wa serikali juu ya jambo hilo.
Amesema mawazo yanayoendelea kutolewa kuhusiana na katiba hiyo yanabakia kuwa misimamo ya vyama na siyo msimamo wa serikali kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.
“Mimi nikiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kama Serikali hatujawahi kukaa kwenye Baraza la Mapinduzi wala Kikao chochote cha Kiserikali kujadili au kutoa msimamo kuhusu katiba inayopendekezwa, sasa inakuwaje wengine wanasema msimamo wa serikali ni huu”, alihoji Maalim Seif.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, amesema mwaka 2015 ni mwaka wa wanaCUF kufanya maamuzi ya kukiweka chama hicho madarakani kwa kukiwezesha kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mkutano huo, wazee wa CUF makunduchi wamemkabidhi Maalim Seif ufunguo maalum kwa ajili ya kuifungua Zanzibar ambayo wamedai kuwa imekwama kwa zaidi ya nusu karne sasa.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Katibu Mkuu huyo wa CUF alifanya ziara ya kutembelea barza na matawi ya CUF na kupata fursa ya kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika matawi na barza hizo zikiwemo mbili za akinamama.
Kwenye ziara hiyo Maalim Seif ambaye aliambana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, aliwahimiza wanachama wa barza hizo kuanzisha matawi kamili kutoka na idadi kubwa ya wanachama waliyonayo.
Miongoni mwa barza na matawi yaliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi ni pamoja na Barza ya Kizimkazi Dimbani, Barza ya Ukawa ya Nganani, Barza ya Ismail Jussa ya Kitundani, Fatma Ferej Madete Barza na Tawi la CUF Shakani.
Wanachama wapya waliojiunga na CUF kutoka CCM ni pamoja na aliyekuwa mjumbe wa baraza la wazazi Wilaya ya kusini Bw. Yahya Mkongoa Ali na aliyekuwa muhamasishaji wa CCM katika eneo hilo Bi. Kihamba Ali Ronge.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni