Jumatatu, 30 Machi 2015
MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR, MAALIM SEIF AKUTANA NA BALOZI WA KUWAIT NCHINI
Na: Khamis Haji, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad
amesema Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Kuwait, ikiwemo njia bora ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ili iweze kuwanufaisha wananchi wote.
Maalim Seif amesema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem Ibrahim Al- Najem ambaye alifika ofisini kwake kujitambulisha.
Maalim Seif amesema Kuwait ina uzoefu mkubwa katika sekta ya mafuta na gesi na ni vyema wakati huu ambapo Zanzibar ina matumaini makubwa ya kuwa na maliasili hiyo, inaweza kupata uzoefu mkubwa juu ya Sera ya matumizi ya mafuta na gesi kutoka Kuwait.
Amesema sekta hiyo inahitaji umakini wa hali ya juu kwa sababu mafuta na gesi ni maliasili zisizorejesheka, mipango imara ya matumizi ya mapato yake inahitajika, ili nchi iweze kujiendesha vizuri na iwe na uchumi imara hata baada ya maliasili hiyo kumalizika.
Aidha, Maalim Seif amemueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inazo fursa nyingi za uwekezaji vitegauchumi ambazo zinaweza kutumiwa vyema na wafanyabiashara wa Kuwait.
Naye Balozi Najem amesifu uhusiano wa miaka mingi uliopo kati ya Kuwait na Zanzibar na kuahidi akiwa katika nafasi hiyo ya Balozi nchini Tanzania atahakikisha unazidi kuimarika.
Amemuahidi Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa atawashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi yake kuja Zanzibar kuona maeneo ambayo wanaweza kuyatumia kwa uwekezaji na kufungua miradi yao.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni