BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limekubali kuanza
ushirikiano na uhusiano mzuri na Chama cha Bloggers Tanzania (TBN) mara
kitakapo maliza mchakato wa usajili wake na kutambulika rasmi kisheria.
MCT imesema kwa hatua ya kwanza itafanya mazungumzo na viongozi wa TBN
na kujadiliana namna gani ya kuisaidia TBN.
Kauli
hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa MCT,
Kajubi Mkajanga alipokuwa akizindiwa hafla ya kwanza ya mwaka 2015 ya
wamiliki na waendeshaji wa blogu na mitandao mingine ya kijamii
iliyofanyika katika Hoteli ya Serena.
Katibu
huyo Mtendaji wa MCT alisema kwa maendeleo ya sasa ya teknolijia ya
habari na mawasiliano ni vigumu kuzitenga blogu kama vyombo vya habari,
hivyo kuahidi kushirikiana na TBN kuhakikisha inafikia malengo yake ya
kuwaunganisha bloggers na kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili.
Alisema
MCT inasubiri TBN ipate usajili kisheria toka mamlaka husika serikalini
na baada ya zoezi hilo itaanza kushirikiana maramoja na chombo hicho
kilichoanzishwa kuwaunganisha wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya
kijamii nchini na wale wanaofanya shughuli za nje ya nchi.
"...MCT
ipo tayari wakati wowote kuanza kushirikiana nanyi kikazi,
tunachosubiri ni TBN kusajiliwa rasmi...mtakapo maliza usajili tu njooni
ofisi, tutazungumza na viongozi wenu ili kujua nini cha kuwasaidia.
Naombeni msichelewe tuanze hili mara moja," alisema Kajubi Mkajanga
akizungumza na wana-TBN kabla ya kuzinduwa sherehe hiyo.
Awali
akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa TBN, Joachim Mushi alisema
kwa sasa mitandao ya kijamii imekuwa ikitekemewa na kundi kubwa la jamii
katika kusambaza taarifa kwa haraka licha ya uwepo wa changamoto kadhaa
ndani ya tasnia hiyo.
Alisema pamoja na mambo
mengine, TBN imeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha waendeshaji na
wamiliki wa blogu pamoja na mitandao mingine ya kijamii, na pia
kuhakikisha wana-TBN wanapata fursa ya kujifunza zaidi maadili ya tasnia
ya habari na mawasiliano ili kufanya kazi zao kiufanisi zaidi.
Aidha
aliishukuru Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania kwa kusaidia
kufanikisha tukio la kukutana 'bloggers', pamoja na Benki ya NMB na
makampuni mengine ya Coca Cola, AIM Group na kampuni ya huduma za
intanenti ya Raha kufanikisha tukio hilo la kuwaleta pamoja bloggers wa
Tanzania.
Akisoma risala ya wana-TBN kwa mgeni
rasmi, Mjumbe wa TBN, Henry Mdimu alisema licha ya blogu kuwa chanzo
kikubwa cha habari na mstari wa mbele kuwafikishia wananchi habari kwa
haraka zaidi lakini bado zimekuwa hazitambuliwi na mamlaka zinazosimamia
na kutetea tasnia nzima ya habari.
"...Pamoja
na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na 'bloggers' na waendeshaji wa
mitandao ya kijamii, bado hawatambuliki rasmi na mamlaka husika pamoja
na taasisi zinazohusika na usimamizi wa tasnia hii likiwemo Baraza la
Habari Tanzania (MCT), Idara ya Habari (Maelezo), MISA-Tan na hata Mfuko
wa Ruzuku kwa Vyombo vya Habari nchini (TMF).
"..Tunasema
hivi maana tunaona kwa namna moja ama ingine wadau hawa muhimu
hawajumuishwi katika harakati au michakato yoyote ile mnayoifanya kwenye
tasnia hii. Mfano kupata semina za MCT, kupewa vitambulisho (Press
card), kushiriki katika mafunzo na hata mashindano ya kila mwaka ya
wanahabari yanayoandaliwa na MCT," alisema Mdimu akisoma risala ya TBN
mbele ya mgeni rasmi Bw. Mkajanga.
Kwa upande
wa waalikwa rasmi kutoka ubalozi wa Marekani wakizungumza katika hafla
hiyo kupitia kwa mwakilishi wao ameahidi kuisaidia TBN katika programu
mbalimbali ili kuchochea uhuru wa habari nchini Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni