Mahakama ya Wilaya ya Dodoma jana
ilimwachia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson
Minja kuendelea na dhamana yake baada ya kujiridhisha kuwa hakuvunja
masharti ya dhamana yake tangu aliapoachiwa kwa dhamana Januari 28
mwaka huu.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Dodoma, Rhoda Ngimilanga alisema kuwa ameridhishwa na
upande wa utetezi kuwa mshtakiwa hajawahi kuvunja masharti ya dhamana
yake tangu alipoachiwa kwa dhamana Januari 28 mwaka huu.
Awali mwendesha mashtaka mwandamizi
wa serikali, Rose Shio aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umeshakamilika ambapo April 9 itaanza kusikilizwa kwa usikilizwaji wa
awali.
Hata hivyo aliiomba mahakama hiyo
kuendelea kuzuia dhamana ya Mshtakiwa kwa kuwa bado hapakuwa na
utulivu wa amani nje kutokana na wafanyabiashara kuendeleza migomo ya
kufungua maduka yao pamoja na kugoma kuendelea kutumia mashine za
kieletroniki za Efds.
“Pamoja na kukamilika kwa
upelelezi wa kesi hiyo lakini mshtakiwa ameendelea kukiuka masharti
ya dhamana aliyopewa Januari 28 mwaka huu kwa hiyo tunashauri
mahakama iendelee kuzuia dhamana ya mshtakiwa hadi pale hali ya amani
itakapotengemaa katika mji wa Dodoma,” alisema Shio na kuongeza
kuwa, “Bado kuna hali ya tahadhari katika mji wa Dodoma, biashara
bado haziendelei na pia bado kuna mgomo wa kufungua maduka, na
utumiaji wa mashine za kukusanya kodi za efds ambapo kwa sasa hali
imekuwa ni mbaya zaidi kwa hiyo tulikuwa tunashauri kuwa mshtakiwa
arudi ndani hadi hali ya usalama itakapotengemaa.”
Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa,
Godfrey Wasonga aliipinga hoja ya wakili wa serikali kwa kusema kuwa
mshtakiwa huyo ana haki ya kupata dhamana kama ilivyo kwa makosa
mengine ya jinai na kwamba kuendelea kumshikilia ni kuvunja katiba ya
nchi.
“Napenda kuiambia mahakama yako
tukufu kuwa tangu mshtakiwa aachiwe kwa dhamana hajawahi kuvunja
sharti hata moja la dhamana yake,” alisema Wasonga
Alisema na hoja ya serikali kuwa
anaitisha mikutano ya kuwazuia wafanya biashara kugoma kutumia
mashine za kieletroniki za efds alisema kuwa katika masharti ya
dhamana yake hakukatazwa kuitisha mikutano na wala hajawahi kuwazuia
wafanyabishara nchini kutumia mashine za kukusanya kodi za efds.
Pia alisema kuwa hoja ya kwamba
mshtakiwa aendelee kukaa gerezani mpaka amani itakaporejea alisema
kuwa jukumu la kulinda amani ya mahali husika ni la serikali na siyo
jukumu la Minja.
“Sasa kama Minja ataendelea kukaa
ndani atajuaje kama Tabora, Tanga, Arusha na Mbeya maduka
yamefunguliwa?” alihoji Wasonga na kuongeza kuwa,
“Mheshimiwa hakimu najua kuwa
mahakama ndiyo chombo pekee cha kutoa haki na usiendelee kusikiliza
taarifa za umbea umbea kutoka kwa wakili wa serikali.”
Aliishauri mahakama kumwachia huru
mshtakiwa kwa masharti ya mwanzo ili aendelee kufanya shughuli zake.
Masharti ya mwanzo ya dhamana
aliyopewa Minja ni kuwa na wadhamini watatu ambapo mmoja kati ya hao
ni lazima awe ni mfanyakazi wa serikali ambaye anaishi mkoani Dodoma.
Akijibu hoja hizo Hakimu Ngimilanga
alisema kuwa hoja ya wakili wa serikali kuwa Minja alikuwa anaitisha
mkutano ya kuwazuia wafanyabishara haina mashiko kwa kuwa kama
alifanya hivyo sheria inasema kuwa angekamatwa muda huo huo na kwamba
hilo halikuwa miongoni mwa masharti ya dhamana yake.
Alisema kuwa mshtakiwa ataendelea
kuwa nje kwa dhmana hadi April 9 mwaka huu ambapo kesi hiyo itatatjwa
tena kwa usikilizwaji wa awali.
Mwisho.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni