Jumatano, 22 Aprili 2015
SERIKALI YAFANIKIWA KUWAREJESHA NCHINI WATANZANIA 18 KUTOKA YEMEN KUFUATIA MAPIGANO YANAYOENDELEA NCHINI HUMO
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Watanzania hao Bw. Sabri Abeid Almaghi ambaye alikua anafanya biashara nchini Yemen amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa namna ya pekee kwa kuwajali wananchi wake bila kujali wapo nchini au nje ya nchi na kutoa msaada kwa wakati.
“Tunaishukuru sana serikali yetu ya Tanzania kwa jinsi ambavyo wanajali wananchi wake bila kujali wapo ndani au nje ya nchi, kweli kama sio jitihada za ubalozi wetu pale mjini Muscat, sijui leo tungekua katika hali gani, tunaomba shukrani zetu mzifikishe kwa Rais Kikwete, Waziri Membe na wahusika wengine wote waliofanikisha kuturejesha nyumbani” alisema Mzee Saleh Mbaraka Jabri mmoja wa watanzania hao waliorejea kutoka Yemen.
Aidha, akizungumzia hali ya usalama ilivyo nchini Yemen, Bw. Almaghi amesema kuwa hali ni mbaya sana kufuatia mapigano ya anga yanayoendelea hivi sasa na muda wowote yataanza mapigano ya ardhini. Aidha amesema kuwa kufuatia hali hiyo huduma zote za kijamii pamoja na biashara zimesimama.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea watanzania hao Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Bi. Mindi Kasiga amesema mpaka hivi sasa watanzania ambao wamesharejeshwa nchini kutoka Yemen ni 23, kati ya Watanzania 69 ambao wamejiandikisha na jitihada zinaendelea.
“Awamu ya kwanza ya Watanzania waliorejeshwa na serikali kutoka nchini Yemen ni familia moja ya watu watano ambao walirudi wiki chache zilizopita” alimalizia Bi. Mindi Kasiga.
Hivi karibuni Serikali kupitia Waziri wa Mambo na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe ilitangaza kuwarejesha nchini Watanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni