Na, Himid Choko, BLW.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanatarajiwa kuanza kuchambua Bajeti ya Serikali na ile ya kila wizara kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 kuanzia Alkhamis ijayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Afisini kwake Chukwani nnje Kidogo ya Mji wa Zanzibar, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahya Khamis Hamad amesema maandalizi yote kwa ajili ya shughuli hiyo tayari yamekamilika.
Amesema shughuli zote za kupitia Bajeti hizo zitafanyika katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani, na zitaanza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2015/2016 na baadae Waziri wa Fedha kuwasilisha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 2015/2016 mbele ya Kamati ya Wenyeviti ya Baraza la Wawakilishi, siku ya Alkhamis ya Tarehe 30/5/2015.
Katibu Yahya amefafanua kwamba Kamati hiyo ya Wenyeviti inaundwa na Wenyeviti wa Kamati zote saba za Kudumu za Baraza la Wawakilishi na itajadili Bajeti hiyo siku ya Jumamosi ya tarehe 02/05/2015 na Jumapili ya tarehe 03/05/2015 na hatimae bajeti hiyo itawasilishwa katika Baraza zima la Wawakilishi Jumatano ya tarehe 13/05/2015.
Aidha amesema kwa upande wa Bajeti za Kisekta, Kamati za kudumu zitaanza kujadili Bajeti za Wizara zinazozisimamia kuanzia Jumatatu ya tarehe 04/05/2015 hadi Alkhamis ya tarehe 07/05/2015 na baadae zitawasilishwa katika Baraza zima wakati wa Mkutano wa Bajeti.
Katibu huyo wa Baraza la Wawakilishi amezidi kufafanua kwamba, Utaratibu wa kuwasilisha, kujadili, na kupitisha bajeti ya serikali kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar umewekwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya 1984 na umefafanuliwa kwa upana zaidi kwenye Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012.
“Makadirio ya jumla ya Bajeti ya Serikali kwanza hupelekwa kwenye Kamati ya Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa Kanuni ya 95 (1) (Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012) na baadae ndipo huwasilishwa kwenye Baraza’’ Alisema Katibu Yahya.
Yahya aliendelea kusema kwamba “Mapendekezo ya bajeti ya kila Wizara kwanza hupelekwa kwenye Kamati husika ya kisekta kwa mujibu wa Kanuni ya 96 (1) na baada ya Kamati husika kumaliza kazi ya kushughulikia mapendekezo hayo ndipo huwasilishwa kwenye Baraza na Waziri mwenye dhamana ya Wizara husika au Kaimu wake.”
Amesema bajeti ni nyenzo muhimu na muhimili wa maendeleo na ustawi wa jamii hivyo amewaomba wananchi kufuatilia mchakato wa Bajeti kwenye Baraza na kushirikiana ipasavyo na Wawakilishi wao na wahakikishe kwamba bajeti inaakisi maisha yao ya kila siku kulingana na wakati uliopo.
Aidha amesema hivi sasa ni wakati muwafaka wa wananchi kuwatosheleza wawakilishi wao pamoja na Wajumbe wenyewe kufanya utafiti ili hatimae kuhakikisha kwamba maudhui ya mijadala ya shughuli za kila Wizara yanalenge juu ya Sera na Sheria za Fedha, Utawala na Utendaji bora wa shughuli za Umma.
“Pamoja na kuzingatia hizo sera na masuala ya Malengo ya Milenium Mijadala yao pia inatakiwa ijikite katika kuwasilisha maoni na mitizamo ya wananchi pamoja na kero zinazowakabili katika kutathmini vipaumbele vya Bajeti hiyo ” alisema Katibu Yahya.
Mkutano ujao wa Baraza la Wawakilishi ambao utajadili Bajeti, unategemewa kuanza Jumatano ya tarehe 13/05/2015 na kuchukua takriban mwezi mmoja na nusu.
MWISHO.
Imetolewa na.
Himid CHOKO,
O777436016 BLW, zanzibar,
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni