.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 9 Juni 2015

DK. SHEIN ASEMA, KUVUMILIANA NA KUHESHIMU KATIBA NDIYO SIRI YA MAFANIKIO YA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema uvumilivu wa kisiasa na kuheshimu Katiba na sheria ndio siri ya mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa

Akijibu maswali kutoka kwa watanzania wanaoishi nchini Ujerumani hapo jana, Dk. Shein alisema yeye binafsi na viongozi wenzake serikalini wameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.

“sisi sote tunaridhika na mafanikio yetu katika kuendesha serikali pamoja na kuwepo na changamoto za hapa na pale” alisema na kuongeza kuwa kikubwa kwao ni kuwa wamekuwa wakivumiliana kwa kiwango kikubwa.

Alifafanua kuwa Katiba ya Zanzibar imeweka misingi imara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Mfumo wa umoja wa kitaifa na yeye amekuwa mfano wa kuheshimu Katiba hiyo wakati wote anapotekeleza majukumu yake.

Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imefanikiwa kutekeleza malengo yake kwa kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanakuwa na utengamano wa kisiasa na kurejesha amani na utulivu ili kutoa fursa ya kushughulikia masuala ya maendeleo yao na nchi yao.

“Tumeweza kufanya mambo mengi ya maendeleo ambayo wengi hatukuyatarajia” alisema Dk. Shein na kubainisha kuwa hali hiyo ya utulivu na amani imevutia sio tu washirika wa maendeleo kusaidia Zanzibar lakini hata wawekezaji wakubwa duniani sasa wamejenga imani na matumaini hivyo kuendelea wanawekeza Zanzibar.


Kuhusu kuendelea kuwepo kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya mfumo Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi Mkuu, Dk. Shein alieleza kuwa hilo ni suala la kikatiba hivyo litaendelea kuwepo hadi hapo wananchi watakapoamua vinginevyo.

Akizungumza kuhusu ziara yake nchini humo, Dk. Shein alisema lengo kuu ni kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ujerumani kwa upande mmoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ujerumani kwa upande mwingine.

“Ni uhusiano wa kihistoria ulioanza karne nyingi na dhamira yetu ni kuuimarisha kwa kiwango cha juu”Dk Shein alieleza.

Akijibu swali kuhusu Muungano Dk. Shein alieleza kuwa Muungano halikuwa tukio la kukurupuka/kubahatisha bali ni matokeo ya historia ya watu wa Zanzibar na Tanganyika.

“ni suala la kihistoria kati ya watu wa pande mbili hizi-watu wenye asili moja, mila na silka moja na uhusiano wa damu”alieleza na kusisitiza kuwa suala la Mungano halikuwa matakwa binafsi ya viongozi.

Aliwataka watanzania hao kuendelea kujituma kwa kufanyakazi kwa bidii na kwa wale wanaosoma wajitahidi kupata elimu ili waweze kutengeneza masiha yao ya leo na baadae.

Dk. Shein aliwakumbusha watanzania hao kuhakikisha wanatafuta fursa nchini humo ili kuendeleza nyumbani na pia kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ili waendeleze sifa nzuri ya nchi yetu na wao waweze kuendelea kuishi na kufanyakazi bila ya matatizo.

Awali akizungumza kumkaribisha Mhe Rais, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Philip Marmo alieleza kuwa kati ya watazania 525 wanaoishi katika karibu nchi kumi zilizo chini ya ubalozi huo wengi wao wanaishi nchini Ujerumani.



Alieleza kuwa watanzania hao wamekuwa wakiiwakilisha nchi yetu vyema kwa kuonesha mwenendo na tabia nzuri kwa kufuata sheria na taratibu nchini humo hivyo kutokuwepo kabisa matukio ya mtanzania kutiwa magerezani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa watanzania nchini Ujerumani (UTU) bwana Mfundo Peter Mfundo alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 umoja huo umeandikisha wanachama 360.

Alibainisha kuwa lengo la UTU ni kuwakusanya pamoja watanzania nchini humo ili kufahamiana na kusaidia wakati wa shida, kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuchangia maendeleo nyumbani kwa kutafuta fursa zilizopo nchini Ujerumani na nchini Tanzania pamoja na kuwandaa watoto wao kuifahamu asili yao huko nyumbani.

Dk. Shein anaendelea na ziara yake leo ambapo atakwenda katika mji wa Postdam kutembelea skuli ya Burno-H- Burgel ambayo ina uhusiano na skuli ya Mwanakwerekwe ya mjini Unguja.

Wakati wa mchana atatembelea makumbusho mjini Berlin, baadae jioni atakutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaowakilisha nchi zao nchini Ujerumani.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni