Na Asteria Muhozya, Tanga.
Kampuni za uchimbaji madini, utafutaji mafuta na gesi wakiwemo wachimbaji wadogo nchini, wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira wakati wanapotekeleza shughuli zao, ili kuwezesha rasilimali zinazopatikana ardhini ziweze kuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Rai hiyo imetolewa na na Mhandisi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ephraim Mushi wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Tangamano Jijini, Tanga.
Mhandisi Mushi ameeleza kuwa, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ni muhimu mahitaji yao yakaenda sambamba na rasilimali zilizopo.
“Nafahamu uelewa wa makampuni ya uchimbaji madini na utafutaji wa mafuta na gesi katika usimamizi na kutunzaji wa mazingira ni mkubwa, kwani tayari kampuni hizo zina mpango wa usimamizi mazingira ambao umeeleza masuala yanayopaswa kuzingatiwa, lakini bado wanapaswa kuzingatia jambo hili wakati wote kutokana na umuhimu wa wake”, alieleza Mushi.
Kuhusu wachimbaji wadogo ameeleza kuwa, bado wanafanya shughuli zao za uchimbaji bila kuzingatia sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira. “Wachimbaji wadogo bado hawazingatii suala hili lakini Wizara inafanya jitihada mbalimbali za mara kwa mara kuhakikisha wachimbaji wanafuata taratibu ikiwemo kuwaelimisha kuhusu usalama na mazingira”,aliongeza.
Hivyo, amewataka wachimbaji wadogo kuwa na mpango wa utunzaji mazigira kwa kuwa utaonesha namna ya kuhifadhi na kutunza mazingira na hivyo kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni husika.
Akieleza zaidi kuhusu jitihada zinazofanywa na wizara katika kusimamia masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira, hususan katika sekta za nishati na madini, ameeleza kuwa, Wizara imeshatoa mafunzo kadhaa kuhusu masuala hayo kwa maafisa mazingira mazingira wa halmashauri katika Wilaya mbalimbali za mikoa ya Mwanza, Iringa na Mbeya kuhusu sheria na kanuni za madini na athari za uchimbaji usiozingatia uhifadhi mazingira.
Vilevile ameongeza kuwa, wizara mafunzo mengine ni pamoja na mpango kazi wa mazingira wa wizara ambapo maafisa mazingira hao wanatakiwa kuingiza masuala ya madini kwenye mpango kazi yao. Mafunzo hayo pia yanatarajiwa kuendelea kufanyika katika miningine katika mwaka wa fedha ujao.
Aidha, ameeleza kuwa, wizara imekuwa ikishirikiana na taasisi kadhaa zenye uhusiano wa masuala mazingira kama vile Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na wizara nyingine katika masuala yanayohusu miradi ya nishati na madini jambo ambalo limeleta matokeo mazuri kwa kuwa miradi yote ya nishati na madini haiwezi kuanza bila kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira.
Siku ya mazingira duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 1 - 5 Juni, ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu “ Ndoto Bilioni Saba. Dunia Moja. Tumia Rasilimali kwa Uangalifu”. Aidha, maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na tarehe 1 Mei,2015, na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samwel Sitta (Mb)kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt . Mohamed Gharib Bilal.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni