Ofisa mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Dainius Puras akizungumza kwenye mkutano huo.
Ofisa Habari wa Kituo cha Taarifa cha Umoja wa Mataifa (UN), Stella Vuzo
akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari vilipozungumza na
viongozi wawakilishi walioshiriki katika mkutano huo.
TANZANIA inajivunia mafanikio makubwa ya kupunguza
idadi ya vifo vya wajawazito pamoja na idadi ya watoto chini ya miaka
mitano wanaopoteza maisha kila mwaka. Mafanikio hayo yameifanya Tanzania
kutolewa mifano kimataifa ikiwa ni kati ya nchi zilizovuka malengo ya
kupunguza idadi hiyo vifo iliyojiwekea kuzifikia.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Vizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Donan Mmbando katika hotuba yake iliyosomwa na mwakilishi wake akifungua
mkutano wa majadiliano na wadau mbalimbali wa utetezi wa haki za
binadamu unaokutana kuangalia namna ya kupunza idadi ya vifo
vinavyotokana na uzazi na vile vya watoto chini ya miaka mitano.
Majadiliano
hayo yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili huku yakijikita
kuangalia namna wadau wa haki za binadamu wanavyoweza kuchangia katika
kuboresha huduma za afya na hatimaye kumlinda mtoto chini ya miaka
mitano na vifo kwa ujumla.
Dk. Mmbando alisema
Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi na watoto, kutoka idadi ya
vifo 166 vilivyokuwa vikitokea kwa kila akinamama 1,000 wanaojifungua
mwaka 1990 na kupungua hadi kufikia idadi ya vifo 54 kwa kila akinamama
1,000 mwaka 2012.
Alisema mafanikio hayo ni
makubwa kwani yalivuka malengo iliyokuwa imejiwekea, huku nchi ikitolewa
mfano kati ya mataifa yaliyofanikiwa kiasi kikubwa kupungu vifo vya
kesi za uzazi na huduma za afya kwa ujumla.
Aidha pamoja na
hayo alisema bado kuna changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma za
afya kutoka eneo moja hadi lingine, hasa maeneo ya vijijini jambo
ambalo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inakabiliana na
changamoto hizo.
Alizishukuru taasisi za Umoja
wa Mataifa (UN) kwa msaada zinazoutoa kupitia taasisi zake mbalimbali
kuisaidia Serikali ya Tanzania kuboresha huduma za afya katika nyanja
tofauti, jambo ambalo ndio chachu ya mafanikio zaidi.
Awali
akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwakilishi wa UNICEF
Tanzania, Dk. Jama Gulaid, aliipongeza Tanzania kwa mafanikio makubwa
iliyoyapata katika kupunguza vifo vya uzazi pamoja na watoto chini ya
miaka mitano na pia kuwalinda watoto katika kupata huduma bora za afya.
Aliongeza
kuwa mafanikio hayo yanatokana na uongozi mzuri wa Serikali pamoja na
nia thabiti ya viongozi kutambua tatizo na utayari wa kulisimamia
kuhakikisha linapata ufumbuzi, lakini pia usalama wa raia na shughuli
zao.
“…Napenda nitumie nafasi hii kuwasilisha
shukrani na dhati kutoka UNICEF kwa Wananchi wote wa Tanzania kwa
kuendelea kulinda haki za watoto, nawapongeza kinamama, nawapongeza
kinababa na viongozi kwa ujumla kwa kulilinda hili…kimsingi tunaitaji
mchango wenu kufanikiwa zaidi,” alisema Dk. Gulaid akiwahutubia
washiriki wa mkutano huo.
Mkutano huo wa siku
mbili unashirikisha wajumbe na wawakilishi kutoka taasisi za kimataifa
na kitaifa zinazoshughulikia masuala ya haki za binadamu, afya na watoto
umeandaliwa na Tume ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
kwa kushirikiana na Taasisi za Umoja wa Mataifa.
*Imeandaliwa na Mtandao wa www.thehabari.com














Hakuna maoni :
Chapisha Maoni