TIMU ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 15, jioni ya leo imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kombaini ya vijana chini ya umri wa 17 ya mkoa wa Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini hapa.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi dakika 45 za kwanza zilimalizika U15 wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Timoth Maziku dakika ya 17 kwa guu la kulia akimalizia krosi ya Nahodha Issa Abdi.
Baada ya bao hilo, Mbeya Kombaini walitulia na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwa timu ya taifa, hali ambayo ilifanya timu hizo zishambuliane kwa zamu huku pia vijana wakionyesha uwezo wa kuridhisha.
Dakika ya 72, Albinius Haule almanusra aisawazishie bao Mbeya kama si shuti lake zuri la kitaalamu alilopiga kutoka umbali wa mita 25 kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.
Nahodha Issa Abdi aliifungia timu ya taifa bao la pili dakika ya 82 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Timoth Maziku kuangushwa nje kidogo ya boksi na Richard Paul.
Emmanuel Ntindi wa Mbeya alijifunga dakika ya 87 katika harakati za kuokoa krosi ya Asad Ally dhidi ya Maziku.
Mchezo ulikuwa mzuri, vijana walionyesha ufundi wa hali ya juu na Mbeya pamoja na kufungwa, walicheza vizuri na kilichowakwamisha kupata japo bao moja ni uhodari wa kipa Kelvin Deogratius wa U15 ya taifa.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kesho jioni kwenye Uwanja Sokoine na mapema Jumanne U15 watarejea Dar es Salaam na vijana kuvunja kambi hadi watakapokusanyika tena mwishoni mwa mwezi ujao kwa safari ya Zanzibar kwa michezo mingine ya kujipima.
Vijana hao walio chini ya kocha Bakari Shime wanaandaliwa kwa ajili ya kucheza mechi za kufuzu Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2017 na kila wiki ya mwisho wa mwezi watakuwa wakikutana kwa mazoezi na michezo ya kujipima nguvu.
Kikosi cha Mbeya Kombaini kilikuwa; Edward Mwakyusa, Josephat Frank, Seif Gabriel, Emmanuel Ntindi, Richard Paul/Hassam Abdallah dk87, Goodluck Ezeria, Amiri Nyeo, Castro Issa, Albinius Haule, Biya Stephen na Daniel Samson/Castro Moses dk73.
Tanzania U15; Kelvin Deogratius, Kibwana Ally, Faraji John, Maulid Salum, Ally Hussein, Athumani Maulid/Rashid Kilomtola dk75, Robert Philipo/Morris Michael ‘Chuji’ dk86, Asad Ally, Timoth Joseph, Issa Abdi na Juma Zubeiry/Juma Juma dk61.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni