.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 24 Juni 2015

UNESCO KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI JAMII YA KIMASAI NGORONGORO



 
                                                       *Imeandaliwa na www.thehabari.com,Ngorongoro. 
 
SHIRIKA la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania linatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha sanaa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiliamali wa bidhaa zinazotokana na mifugo kwa akinamama na wasichana kutoka Kata tano za Wilaya ya Ngorongoro kama jitihada za kuongeza kipato kwa familia za jamii ya Wamasai.
 
Akitoa maelekezo ya mradi huo juzi katika Kijiji cha Ololosokwan mbele ya Katibu Tawala, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kristian Kileo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues alisema mradi huo unatarajia kutekelezwa kuanzia Mwezi Agosti, 2015.
 
Bi. Rodrigues alimueleza Kileo kuwa mradi huo unajumuisha ujenzi wa kituo cha kisasa cha sanaa ambacho kitatumiwa na wajasiliamali wa jamii ya Kimasai kwa ajili ya kuuza bidha zao za asili mbalimbali kwa watalii wanaofika kutembelea vivutio anuai vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro inayozunguka vijiji hivyo.
 
Akifafanua zaidi juu ya mradi huo, Ofisa Mradi Utamaduni wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Rehema Sudi alisema mradi huo utajumuisha mafunzo ya ujasiliamali juu ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi, pembe za ng'ombe pamoja na shanga ili kuziongezea thamani na kuuzwa kwa watalii anuai wanaotembelea vivutio na kukuza vipato vya familia hasa akinamama.
 
Bi. Sudi aliongeza kuwa kata zinazotarajia kunufaika na mafunzo na ujenzi wa kituo hicho cha kisasa kwa ajili ya mauzo ya bidhaa hizo za asili za Wamasai ni pamoja na Kata za Ololosokwani, Arash, Soit Sambu, Oloipili na Kata ya Aoliani Magaidulu zote za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
 
"...Mradi huu utajumuisha akinamama na wasichana kutoka kata tano ambazo ni Ololosokwani, Arash, Soit Sambu, Oloipili na Kata ya Aoliani Magaidulu, tutawapatia mafunzo juu ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na ngozi na pembe za ng'ombe pamoja na shanga ikiwa ni hatua ya kuziongezea thamani kisha kuziuza kwa watalii ambao wanatembelea vivutio vya utalii eneo hili hasa Kijiji cha Ololosokwan," alisema Ofisa Mradi Utamaduni Unesco, Bi. Sudi.
 
Alisema wataalam na wabunifu wataletwa katika vijiji vya mradi na kutoa mafunzo kwa akinamama na wasichana kabla ya ujenzi wa kituo maalumu ambacho kitatumiwa na wanufaika wa mafunzo hayo kama eneo la kuuzia bidhaa zao ikiwa ni sehemu pia ya kulinda na kukuza tamaduni za jamii ya Wamasai. "...Tutazunguka na kutoa mafunzo juu ya ubunifu na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za ngozi, pembe za ng'ombe pamoja na shanga na kutengeneza bidhaa za asili kwa ajili ya kuziuza kwa wateja hasa watalii," alisema Bi. Sudi.
 
Hata hivyo Ofisa huyo mradi Utamaduni wa UNESCO alisema sehemu ya maandalizi ya mradi huo unaotekelezwa kwa msaada wa UNESCO pamoja na washirika wengine ambao ni Umoja wa Ulaya (EU) na Chuo Kikuu cha Liechtenstein na pia Chuo Kikuu cha Ardhi cha Dar es Salaam imeanza kutekelezwa tangu Februari 2015.
 
Mbali na mradi huo UNESCO pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa Kijiji cha Dijitali, ambao unajumuisha ujenzi wa Kliniki ya kisasa ya matibabu ya macho, Kliniki ya kisasa ya matibabu ya meno pamoja na huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa kutumia fipimo vya 'X-Ray' na 'Ultra-sound' na shule ya kisasa kwa ajili ya mafunzo anuai katika Kijiji cha Ololosokwan huduma itakayosaidia jamii za wafugaji maeneo ya Ngorongoro.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni