WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ambaye pia ametangaza nia ya kuwania urais
wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amepata wadhamini1,897 katika wilaya tatu za mkoa wa Rukwa.
Akitangaza idadi ya watu walijitokeza kumdhamini Waziri Mkuu, Katibu
wa CCM wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Bibi Lucy Mfupe alisema
wadhaminini wote hao wametoka katika wilaya tatu za Nkasi, Sumbawanga
Mjini na Sumbawanga Vijijini.
Alisema katika wilaya ya Nkasi, Waziri Mkuu Pinda amepata wadhamini
1,627 wakati katika wilaya mbili za Sumbawanga Mjini na Vijijini amepata wadhamini 270.
Mapema leo asubuhi, Waziri Mkuu alipita katika ofisi ya CCM Wilaya ya
Nkasi na kuwashukuru wananchama wote waliomdhamini. Mchana alifika
ofisi ya CCM wilaya ya Sumbawanga Mjini na kutoa shukrani kwa wadhamini waliokuwa wamefika kwenye ofisi hizo.
Akitoa nasaha zake kwa wakazi hao, Waziri Mkuu aliwashukuru wote waliomdhamini huku akiwaomba waendelee kumuomba Mungu ili aipatie nchi hii kiongozi mwadilifu na mpenda watu na hasa watu wenye hali ya chini.
Alisema ana imani kuwa Chama cha Mapinduzi kitampitisha kiongozi mwenye kutetea maslahi ya wanyonge ili wapate fursa ya kusonga mbele zaidi.
Mchana huu anaelekea Mbozi na Mbeya Mjini.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni