Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole ( pichani kushoto ) kufanya shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015 akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili. Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na maadili awapo jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya kazi ya sanaa kwenye onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.
Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005 limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja tokea tarehe 24/07/2015.
Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.
Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni