Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewashukuru wanachama wa Chama hicho kwa kumuamini na kuendelea kumuunga mkono katika harakati zake za kisiasa.
Amesema kitendo hicho kinadhihirisha kuwa bado wanachama na wananchi wa Zanzibar wana imani naye, na kwamba hatowaangusha na atatekeleza ahadi zote anazozitoa kwa vitendo, iwapo atachaguliwa kuongoza nchi.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Kibandamaiti, ukiwa na lengo la kumpongeza kwa kuchukua fomu ya kugombea Urais kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Maalim Seif amewaeleza wananchi kuwa iwapo atashindwa katika uchaguzi huru na wa haki atakubaliana na matokeo na atakuwa wa mwanzo kumpongeza mshindi, na kuwashauri wagombea wengine kutoa tamko kama hilo, ili kuwapa matumaini mapya wananchi.
Aidha amelishukuru jeshi la polisi kwa kuimarisha ulinzi wakati wote wa kuchukua fomu na katika mkutano wa hadhara, na kulitaka kuendelea na msimamo huo ili liweze kufanya kazi kwa karibu na wananchi.
Amefahamisha kuwa kitendo hicho kinadhihirisha kuwa inawezekana kwa jeshi la polisi kufanya kazi na vyama vya siasa, na kwamba iwapo jeshi hilo linaendelea kufanya kazi zake bila kuingiza utashi wa kisiasa, litaweza kushirikiana na wananchi na kujenga uaminifu kwa Taifa.
Nae Naibu katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Chama hicho kinakusudia kufanya kampeni za kistaarabu na kuweka wazi sera zake bila ya kukaribisha malumbano.
Amempongeza Katibu Mkuu huyo wa CUF kwa uvumilivu wake, licha ya changamoto kadhaa zilizomkabili, na kwamba wakati umefika sasa kwa Zanzibar kupata mabadiliko ya kweli.
Hassan Hamad, OMKR
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni