.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 20 Agosti 2015

BALOZI SEIF ARUDISHA FOMU YA KUWANIA UJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI JIMBO LA MAHONDA


Wakati harakati za uchukuwaji fomu za kuomba kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kwa wanachama wa vyama vya Siasa Nchini ukiendelea walipomaliza kuthibitishwa na vyama zao baadhi ya wanachama hao tayari wameanza hatua ya kurejesha fomu hizo kwa Ofisi za Tume za Uchaguzi za Wilaya baada kukamilisha kujaza fomu hizo.

Zoezi hilo lililoanza rasmi Mnamo Tarehe 17 Agosti mwaka 2015 na watarajiwa wanaohusika wakiingia katika Ofisi za Tume za Uchaguzi za Wilaya kwa makeke wakiambatana na wapambe wao linatarajiwa kuendelea hadi Tarehe 6 Septemba mwaka huu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amerejesha fomu za kuwania kugombea Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Fomu hizo alizochukuwa Tarehe 17 Agosti alizijaza na kukamilisha ndani ya siku tatu na kuzikabidhi kwa Afisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Wilaya ya Kaskazini “B” Nd.Makame Pandu Khamis kwenye Ofisi hiyo iliyopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akikabidhi fomu hizo Balozi Seif alimuhakikishia Afisa huyo wa Tume ya Uchaguzi kwamba kila alichojaza ndani ya fomu hizo ni sahihi wakiwemo wadhamini 48 licha ya utaratibu wa Tume hiyo kuhitaji wadhamini wasiopungua 25.



Akizipokea fomu hizo Afisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Makame Pandu Khamis alisema kwamba jukumu ya Tume hiyo baada ya kupokea fomu zote ni kuhakiki fomu za wagombe wa ngazi zote kwa lengo la kukamilisha taratibu na kanuni zilizowekwa na tume hiyo.

Nd. Makame alisema watendaji wa Tume hiyo watabandika majina ya wagombea wote mbele ya ofisi hiyo baada ya kukamilisha uhakiki ili kuwapa fursa watakaohusika na mchakato huo kuangalia majina yao endapo kama kutakuwa na mapungufu yoyote.

Afisa huyo wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini “B” alieleza kwamba siku ya uteuzi mgombea aliyetimiza masharti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kipengele cha 46 cha Katiba ya Zanzibar baada ya kuchaguliwa atarejeshewa dhamana ya fedha aliyotoa mgombea huyo wakati aliporejesha fomu zake.

Akizungumza na wana CCM waliokusanyika katika Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “B” hapo Mahonda Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwashukuru na kuwapongeza Wanachama wote waliojitokeza kumdhamini katika mchakato huo.

Balozi Seif alisema ushirikiano waliomuonyesha wadhamini pamoja na wanachama wengine waliojumuika hapo ni ishara ya mwanzo mzuri wa Chama cha Mapinduzi kuelekea katika ushindi mkubwa kwenye uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu wa 2015.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni