.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 1 Agosti 2015

BALOZI SEIF ASHUHUDIA KITUO CHA MAFUNZO YA AMALI MKOKOTONI KIKIPOKEA VIFAA MBALIMBALI VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI MOJA

Haiba ya eneo la mbele la Kituo cha Mafunzo ya Aamali kiliopo Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja ambacho hufundisha vijana waliomaliza masomo yao ya Kidatu cha Nne katika fani mbali mbali za ujasiri amali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Uongozi wa Wizara ya Elimu akitembelea majengo ya Kituo cha Mafunzo ya Amali kilichopata vifaa vipya vya kufundishia vilivyotolewa msaada na Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Maalim Mkubwa Khamis Ibrahim wa mwanzo kutoka kushoto akimtembeza Balozi Seif aliyepo kati kati kwenye maeneo tofauti ya Kituo hicho baada ya kupata vifaa vipya vya kufundishia.
Mkuu wa Kituo cha Amali Mkokotoni Maalim Mkubwa akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi chuo hicho kitakavyokuwa na uwezo wa kutengeneza vyombo vya moto kwa mfumo wa kisasa wa Kompyuta.
Balozi Seif akionekana kufarajika baada ya kuonamashine za kisasa za kutengenezea thamani za ofisini na majumbani zilizomo ndani ya Kituo cha Amali Mkokotoni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwapongeza walimu wa Kituo cha Amali Mkokotoni kwa kazi kubwa ya kuwafinyanga vijana katika mazingira ya muelekeo wa kuweza kijitegemea wenyewe badala ya kusibiri ajira za Serikali. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna.  Picha na – OMPR – ZNZ.

Ile dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ya kuanzisha mafunzo ya Amali ili kuwapa fursa ya uhakika Vijana kupambana na changamoto zinazowakabili za ajira Nchini imeanza kuonyesha muelekeo wa matumaini.

Muelekeo huo wa matumaini unafuatia Kituo cha Mafunzo ya Amali kiliopo Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja kupokea Vifaa mbali mbali vya kisasa vya masomo vilivyotolewa msaada ya Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.

Vifaa hivyo vikiwemo vile vya Ufundi wa Magari, Fanicha cha Maofisini, Mafriji, Televisheni na Matrekta vinakadiriwa kugharimu Dola Laki Tano { 500,000 } za Kimarekani sawa na zaidi ya shilingi Bilioni Moja za Kitanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kufanya ziara fupi kuangalia vifaa hivyo ambavyo baadhi yake tayari vimeshaanza kutumiwa na Wanafunzi wa Kituo hicho.


Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Maalim Mkubwa Khamis Ibrahim alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Kituo hicho kwa Kushirikiana na Wizara ya Elimu unafanya juhudi za kuwapata wataalamu waliobobea watakaosaidia kutoka mafunzo kwa walimu wa Kituo hicho waweze kudumu kuvitumia kwa kuwafundisha Wanafunzi wao.

Maalim Mkubwa alisema vipo vifaa vya kutengenezea vyombo vya moto vinavyotumia mfumo wa Kisasa wa Komyuta ambavyo watumiaji wake watalazimika kupata taaluma ya kina.

Akitoa Taarifa kamili ya Kituo hicho baada ya ziara hiyo Maalim Mkubwa Khamis Ibrahim alisema lengo la kuanzishwa Kituo hicho karibu miaka mitatu iliyopita ni kuwapatia mafunzo ya Amali Vijana baada ya kukosa kuendelea na mafunzo yao ya Sekondari.

Alisema Kituo hicho hivi sasa kinafundisha Fani 11 zinazomjengea uwezo wa kujiajiri mwenyewe Mwanafunzi baada ya kumaliza mafunzo yake ya miaka Mitatu akizitaja baadhi ya fani hizo kuwa ni pamoja na Ufundi Magari, Uashi, Uchongaji, Friji,umeme, bomba, uchoraji pamoja na Mapishi.

Maalim Mkubwa alifahamisha kwamba wakati Kituo kiko mbioni kufunga vifaa vya mawasiliano ili kwenda katika mfumo wa kisasa mkakati mkubwa wa miaka Mitano umeandaliwa katika kuwawezesha wanafunzi wanaomaliza mafunzo yao kufanya Mtihani wa Veta ili kuwajengea uwezo wa elimu wanayoipata ikubalike Kitaifa.

Alifahamisha kwamba mkakati huo umeshasaidia Vijana kadhaa waliopitia Kituo hicho ambao kwa sasa idadi yao imefikia 180 na wengi kati yao wameshaajiriwa katika Taasisi mbali mbali za Umma na hata zile binafsi za ndani ya nje ya Nchi.

Akizungumzia mtazamo wa baadae wa Kituo hicho cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Mkuu wa Kituo hicho Maalim Mkubwa alisema kwamba mpango unaandaliwa wa kuwapatia mafunzo Kituoni hapo wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Pili.

Alisema mkazo utawekwa wa kuwapatia mafunzo Vijana hao ya jinsi ya kuendesha Biashara chini ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa { ILO } kwa Vile Vijana hao wapatao 6,000 wanaomaliza masomo kila mwaka hivi sasa hawaajiriki.

Akitoa shukrani zake kwa juhudi kubwa inayochukuliwa na walimu wa Kituo hicho katika kuwafinyanga wanafunzi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema wakati umefika kwa kila mwana jamii kujifunza kazi yoyote ya amali itakayomuw zesha kuongeza mapato yake na kujikimu Kimaisha.

Alisema hatua hiyo kwa uande mwengine itasaidia kuipunguzia mzigo Serikali Kuu kwa kuagiza baadhi ya vifaa nje ya Nchini ambavyo kama jamii itajipanga vyema vinaweza kutengenezwa hapa hapa Nchini.

Makamu wa ili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza wazo la busara la Uongozi wa Kituo hicho cha Mafunzo ya Amali la kuwaandalia mafunzo Wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Pili.

Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Kituo hicho kwa Kushirikiana na Wizara ya Elimu kwamba ni vyema wanafunzi wanaomaliza mafunzo yao kusaidiwa vifaa vitakavyowapa hamasa ya kuipenda kazi yao wakati watapoamua kujiajiri katika maeneo yao.

Alisema Serikali Kuu inaweza kusaidia kukiwezesha Kituo hicho kununua vifaa hivyo ikiwa kama zawadi kwa kufanikisha vyema mafunzo yao na kianzio kizuri cha mwanzo wa maisha yao.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna alisema vifaa hivyo ni ahadi iliyotolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Kjiislamu ya Irani karibu Miaka mitatu iliyopita.

Waziri Shamuhuna alisema Kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni kilikuwa na upungufu wa vifaa vya mafunzo tokea kilipoanzishwa miaka Mitatu iliyopita ambapo zile ndoto zilizokuwa zikiotwa na Walimu na Wanafunzi wa Kituo hicho sasa zimetimia.

Alisema Walimu wa Kituo hicho sasa watakuwa na uwezo na shauku kubwa ya kusomesha kwa juhudi na maarifa baada ya kupata vifaa tofauti vitakavyokuwa chachu ya matumaini katika siku zijazo.

Othman Khamis Ame
Ofisi yha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni