.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 30 Septemba 2015

LIGI YA MABINGWA BARANI ULAYA, BARCELONA YATAMBA NYUMBANI, ARSENAL NA CHELSEA MAMBO MAGUMU, BAYERN MUNICH YAFANYA KUFURU YA MABAO

Ligi ya mabingwa barani Ulaya imeendelea usiku wa kuamkia leo katika viwanja mbalimbali barani humo, na katika moja ya michezo hiyo FC Barcelona wakicheza nyumbani waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bayer Leverkusen waliosafiri kutoka Ujerumani. 

Pamoja na kuibuka na ushindi huo, Barcelona walijikuta wakitangulia kufungwa katika dakika ya 22 ya kipindi cha kwanza, pale Papadopoulos alipoifungia timu yake bao. 

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika. Ilibidi Barcelona kusubiri hadi dakika ya 80 ya mchezo pale Roberto aliposawazisha bao hilo, na dakika mbili baadaye mshambuliaji mtukutu Luis Suarez akaipatia Barcelona bao la pili nala ushindi katika dakika ya 82
Wakicheza nyumbani katika uwanja wao wa Emirates, washika bunduki wa jiji la London, Arsenal walijikuta wakiwapa huzuni mashabiki wao waliokuwa wamefurika kuwashangilia baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 toka kwa wageni wao Olimpiacos. 

Katika mchezo huo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya uliochezwa usiku wa kumakia leo, Arsenal walipata mabao yao kupitia kwa Theo Walcott katika dakika ya 35 huku Sanchez akifunga bao la pili katika dakika ya 65. 

Mabao ya Olimpiacos yaliwekwa katika nyavu na wachezaji Pardo kunako dakika ya 33, Ospina ( mlinda mlango wa Arsenal ) akiizawadia Olimpiacos bao la pili katika dakika ya 40 na bao la tatu likifungwa na Finnbogason dakika ya 66

Katika mchezo mwingine wa ligi ya mabingwa Ulaya, matajiri wa jiji la London, Chelsea wakicheza ugenini dhidi ya FC Porto waliokuwa katika uwanja wao wa nyumbani huko Ureno walikubali kichapo chepesi cha mabao 2-1. 

Kocha msema hovyo wa Chelsea, Jose Mourihno alishuhudia kikosi chake cha zamani Porto kikimnyima raha baada ya kuacha pointi 3 muhimu huku akiwashuhudia washambuliaji wake wakishindwa kufurukuta katika umaliziaji. 

Mabao ya wenyeji yalifungwa na Andre Andre katika dakika ya 39 huku Maicon akiifungia Porto bao la pili katika dakika ya 52. Bao pekee la kufutia machozi la Chelsea lilifungwa na mshambuliaji raia wa Brazil,
Willian katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza.


Nao Bayern Munich ya Ujerumani ikicheza nyumbani iliweza kuibuka na ushindi wa kishindo baada ya kuisasambua bila chembe ya huruma Dinamo Zagreb kwa mabao 5-0 katika mchezo mwingine wa ligi ya mabingwa barani Ulaya uliochezwa usiku wa kuamkia leo. 

Katika ushindi huo wa kishindo, mshambuliaji mahiri na mwenye uchu wa mabao, Lewandowski alitupia kambani mabao matatu. 

Mabao ya vinara hao yalifungwa na Douglas Costa ( dk 13), Lewandowski akafunga mabao matatu katika dakika za (21, 28 na 55), naye Gotze akafunga moja katika dakika ya (25)




Hakuna maoni :

Chapisha Maoni