Mkutano ukiendelea
Picha na Reginald Philip
Serikali
ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) zimefanikisha jitihada za kuachiwa huru mashehe kutoka
Tanzania waliokuwa wanashikiliwa mateka na moja ya vikundi vya uasi huko
Kivu Kaskazini.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari kuhusu taarifa za kuachiliwa huru kwa Mashehe
hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa taarifa za awali zinaeleza kwamba
mashehe hao ambao walikwenda nchini DRC kwa ajili ya kuhubiri dini
wameachiliwa huru na watekaji jana tarehe 01 Septemba, 2015.
Aliongeza
kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Congo,
Mhe. Anthony Cheche, Mashehe hao kwa sasa wamepelekwa Mjini Goma ambako
taratibu za kukutana nao na kupata undani wao zitafanyika kabla ya
taratibu za kuwarejesha nchini kufanyika.
“Tumepokea
taarifa hizo njema za kuachiliwa huru kwa mashehe hao jana kutoka kwa
Balozi wetu nchini Congo na leo Balozi Cheche anatokea Kinshasa kwenda
Goma waliko Mashehe hao ambapo tutajua idadi yao kamili na masuala
mengine ya muhimu kutoka kwao yatajulikana kabla ya kuanza taratibu za
kuwarejesha nchini” alisema Balozi Mulamula.
Aidha,
Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Serikali
ya Congo kwa ushirikiano wa hali ya juu waliouonesha hadi kufanisha
Mashehe hao kuachiliwa huru wakiwa salama.
Katika
hatua nyingine, Balozi Mulamula alitoa rai kwa Watanzania wanaokwenda
nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kidini, kibiashara au
kutafuta maisha wafuate taratibu ikiwemo kutumia Wizara au Balozi zetu
zilizopo katika maeneo wanayokwenda au karibu na maeneo hayo ili
kuziwezesha Balozi na Serikali kwa ujumla kuwasaidia pale wanapopatwa na
matatizo mbalimbali.
“Napenda
kutoa rai kwa Watanzania wote wanaokwenda nje ya nchi kwa shughuli
mbalimbali kuwasiliana na Balozi zetu kwa kutoa taarifa zao ili
wasaidiwe pale wanapopatwa na matatizo kwani ni jukumu la Balozi kulinda
maslahi ya Tanzania na raia wake katika nchi wanayoiwakilisha, tumieni
Wizara na Balozi zetu kwani ni jukumu letu”, alisisitiza Balozi
Mulamula.
Kwenye
mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya
Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji Kombo alisema kuwa Serikali ya Zanzibar
imefurahishwa na taarifa za kuachiliwa huru kwa mashehe hao ambao
wanatokea Taasisi ya dini ya Tablighi ya Zanzibar.
“Tukio
la kutekwa kwa mashehe hao lilikuwa la kushtusha na kufadhaisha, hata
hivyo Serikali ya Jamhuri na ile ya Zanzibar zililichukua kwa uzito
mkubwa kwa kuwa hawa ni Watanzania wenzetu na tunashukuru jitihada hizo
zimezaa matunda kwa wenzetu hao kuachiliwa huru” alisema Balozi Silima.
|
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni