.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 23 Septemba 2015

MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KWA TIKETI YA CHAMA CHA CUF, MAALIM SEIF AHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI KATIKA MAJIMBO YA KWAHANI NA SHAURIMOYO

                                                                                     Na: Hassan Hamad, OMKR
 

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataviunda upya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuvipatia vitendea kazi na kuimarisha maslahi yao.
 

Amesema vikosi hivyo viliundwa kwa malengo maalum lakini bado havijatimiza malengo yake kutokana na mazingira duni ya kazi zao, jambo ambalo amesema katika uongozi wake atavijengea mazingira bora ili vifanye kazi kwa ufanisi.
 

Maalim Seif ameeleza hayo katika viwanja vya Mkele mjini Zanzibar, wakati akihutubia mkutano wa kampeni kwa ajili ya majimbo ya Kwahani na Shaurimoyo.
 

Amesema vikosi vyote vikiwemo KMKM, JKU, KVZ, Zimamoto na Chuo Cha Mafunzo, vitapatiwa vitendea kazi vya kisasa pamoja na kurekebisha mishahara na maposho yao, ili viweze kulingana na vikosi vya Muungano.
 

Akizungumzia kikosi cha KMKM, Maalim Seif amesema atakibadilisha jina na kukiita kikosi cha ulinzi wa bahari, na kukipatia zana zote zinazohitajika katika utendaji wao, ili kiweze kufuatilia pia usalama wa wananchi wanapokuwa baharini.
 

Kuhusu Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Maalim Seif amesema mbali ya kuliwekea maslahi bora na vitendea kazi vya kisasa, pia ataliwekea mazingira ya kutoa utaalamu wa fani mbali mbali kwa vijana, ili watakapomaliza mafunzo yao waweze kujiajiri.
 

Mapema akitoa salamu za wanawake wa majimbo hayo, Bi Fat-hiya Salim, amewashauri wanawake kumchagua Maalim Seif ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo huduma za afya.

 

Amesema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakihangaikia huduma hizo huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kimaisha, na kwamba iwapo watamchagua Maalim Seif ataweza kutatua changamoto hizo kwa kupatiwa huduma hizo bila ya malipo.
 

Nae kijana Othmani Haji amesema bado vijana wengi wanashindwa kujitokeza hadharani kutokana na kuwaogopa wazazi wao ambao hawajataka kubadilika, lakini watakipigia kura chama cha CUF. Katika mkutano huo Maalim Seif amekabidhi kadi kwa wanachama wapya 26 kutoka majimbo ya Kwahani na Shaurimoyo ambao wamekihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CUF.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni