TANZANIA
imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Dunia kuhusu umuhimu wa
kuongeza Virutubisho kwenye Chakula kwa ajili ya Lishe Bora
utakaofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha kuanzia tarehe 09 hadi 11
Septemba, 2015.
Mkutano
huo ambao utahudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, utafunguliwa rasmi na Mfalme wa Lesotho
Letsie III ambaye ni Kiongozi wa kuhamasisha Lishe na Chakula Bora wa
Umoja wa Afrika.
Mkutano
huo ambao ni wa kwanza kufanyika, utajadili masuala mbalimbali
yanayohusu umuhimu wa kuongeza virutubisho kwenye chakula ikiwemo
vitamini na madini muhimu ili kuwawezesha watu duniani kote kuwa na
afya bora kwa ajili ya uzalishaji na kuleta maendeleo na hatimaye
kuondokana na umaskini.
Pia
Mkutano huu ni sehemu ya jitihada za kimataifa katika kukomesha lishe
duni na utapiamlo uliokithiri katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo
Tanzania.
Aidha,
Mkutano huo utawashirikisha wadau na wataalam mbalimbali kutoka
Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Serikalini. Mashirika hayo ni
pamoja na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la
Afya Duniani (WHO), Shirika la Chakula Duniani (WFP) na Umoja wa Afrika
(AU).
Mkutano
huo umeandaliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana
na Taasisi ya Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) ya
Uingereza.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni