.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 29 Oktoba 2015

MAALIM SEIF AMPINGA MWENYEKITI WA ZEC KUFUTA UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho Mtendeni Zanzibar. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui.
Baadhi ya wafuasi wa CUF wakiwa wamekusanyika nje ya ofisi za CUF Mtendeni kusikiliza kauli za viongozi wao kuhusu maamuzi watakayochukua baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi. 

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya hoteli ya Bwawani kabla ya kutolewa taarifa ya kufutwa kwa uchaguzi. 
(Picha na Salmin Said, OMKR).

                                                                                               Na: Hassan Hamad, OMKR

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Seif Sharif Hamad, amesema tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha la kufuta uchaguzi ni batili kwani halikufuata misingi ya kikatiba wala sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi kuu za Chama hicho zilizoko Mtendeni mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema jopo la wanasheria wa CUF limeliangalia kwa kina tamko hilo na kubaini kuwa halina mashiko ya kisheria.

Akinukuu vifungu vya katiba ya Zanzibar, Maalim Seif amesema kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe saba akiwemo Mwenyekiti ni Mwenyekiti mwenyewe au Makamu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wanne, na kwamba kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi.

Amefahamisha kuwa Chama kimefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa maamuzi hayo ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi hayakuwashirikisha wajumbe wa Tume hiyo, na hivyo yatabakia kuwa maamuzi yake binafsi na sio maamuzi ya Tume.

Amesema kabla ya tamko hilo, Mwenyekiti wa Tume aliwahi kusema kuwa uchaguzi ulikua huru na wa haki, sambamba na waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi wanaoendelea kushikilia msimamo huo.
Amesema pia Mwenyekiti huyo alisimamia kazi ya uhakiki wa matokeo na kutia saini fomu za matokeo yaliyohakikiwa na kuthibitishwa za majimbo 31 ya Unguja na kuyatangaza matokeo hayo.

Hivyo Maalim Seif ameshauri uamuzi huo wa kufuta matokeo ya uchaguzi uekwe pembeni, ili kuruhusu mchakato wa kuhakiki kura uendelee na hatimaye mshindi wa uchaguzi aweze kutangazwa katika siku chache zijazo.

Aidha amesema Mwenyekiti huyo amepoteza sifa ya uadilifu ambayo ni msingi mkuu wa kazi ya Tume ya uchaguzi katika kusimamia maamuzi ya wazanzibari ambao kikatiba ndio wenye mamlaka ya kuwaweka madarakani viongozi wa serikali.

Ameeleza kuwa kutokana na mapungufu hayo Mwenyekiti huyo anapaswa awajibike kwa kujiuzulu, kutokana na hatua yake ya kuiingiza nchi katika mgogoro bila ya kuwepo sababu za msingi.

Amesisitiza wito wake kwa wananchi kuwataka waendelee kuwa watulivu katika kipindi hicho ambacho viongozi wa CUF wanaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo lililojitokeza.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni