Na: Hassan Hamad, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amepiga kura katika kituo cha Garagara Shehia ya Mtoni Kidatu jimbo la Mtopepo.
Maalim Seif ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi CUF, amepiga kura katika kituo hicho mnamo majira ya saa nne asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupiga kura, Maalim Seif amesema ameridhishwa na jinsi wananchi walivyojitokeza kupiga kura, sambamba na utulivu uliokuwepo katika kituo hicho.
Ameelezea matumaini yake ya kupata ushindi katika uchaguzi huo, na kwamba iwapo uchaguzi utafanyika katika hali ya uhuru, haki na uwazi atakubaliana na matokeo ya uchaguzi huo.
“Sina wasi wasi na ushindi na matarajio yangu ni kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 70”, Maalim Seif amewaambia waandishi wa habari.
Hata hivyo amesema tayari zimeripotiwa baadhi ya dosari ikiwa ni pamoja na tuhuma za kuwepo kwa masunduku ya kura feki katika kituo cha skuli ya Jang’ombe.
Amesisitiza haja ya kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki, ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni