Na: Hassan Hamad (OMKR)
Chama Cha Wananchi CUF kimetangaza kutoutambua uamuzi uliotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha, wa kuufuta uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chama hicho Mtendeni mjini Zanzibar, mgombea Urais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Mwenyekiti peke yake hana mamlaka ya kufuta uchaguzi, kwa vile hakuwashirikisha makamishna wa Tume hiyo, na kuuchukulia uamuzi huo kama ni wake binafsi.
Hivyo ameiomba Serikali kuiachia Tume ya Uchaguzi iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na halafu kumtangaza aliyeshinda.
Amesema tayari uhakiki wa matokeo ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya Unguja na majimbo manne ya Pemba ulikua umeshakamilika kabla ya zoezi hilo kusitishwa, na kuishauri Tume ya Uchaguzi kukamilisha zoezi hilo na kumtangaza mshindi.
Aidha ameelezea kusikitishwa na kitendo cha kuchukuliwa kwa nguvu kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Abdulhakim Muhsin Ameir, sambamba na kutoonekana kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo katika kituo cha majumuisho ya matokeo hayo kilichoko Bwawani hadi alipotoa kauli hiyo, pamoja na kutoonekana kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi nd. Salim Kassim Ali.
Baadae Mgombea huyo wa Urais kupitia CUF alizungumza na wafuasi wa Chama hicho nje ya Ofisi hizo za makao makuu Mtendeni, na kuwataka kuwa watulivu na kuendeleza amani wakati Chama kikiendelea kufuatilia haki zao.
Aliwataka wafuasi hao kutokuwa na wasi wasi wa ushindi, na kwamba haki yao hiyo itapatikana ndani ya kipindi kifupi kijacho.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni