WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali inaandaa utaratibu wa namna ya kuweka mfumo mpya wa makazi kwenye eneo la Mishamo, wilayani Mpanda ili wakazi hao waondokane na hali ya kuishi kama wakimbizi.
“Ni lazima tuje na kitu kipya… tumewapa vijiji 16 na kata nne japokuwa najua hazitoshi kulingana na idadi kubwa ya wakazi mliopo kwenye eneo hili. Itabidi Serikali kwa kushirikiana na Mbunge na wadiwani waliopo wakae na kuangalia njia ya kupata kata zaidi,” alisema.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Oktoba 28, 2015) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa eneo hilo waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira Mishamo ili watoe shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa kuwapatia uraia waliokuwa wakimbizi wa Burundi wa mwaka 1972.
Waziri Mkuu alisema kwa sasa eneo lao lina tarafa moja lakini bado haitoshi.
“Mnahitaji kuwa na tarafa mbili au tatu, mnahitaji shule, zahanati na vituo vya afya. Serikali ilishafanya uamuzi kwamba kila kata iwe na shule ya sekondari na kituo cha afya, na kila tarafa lazima iwe na shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita,” aliongeza.
Akipokea shukrani hizo kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu alisema masuala ya maji na umeme katika makazi hayo yanashughulikiwa na Serikali na kwamba muda si mrefu watapatiwa huduma hizo.
Kuhusu barabara, alisema ya kutoka Mpanda kwenda Uvinza itajengwa kwa kiwango cha lami lakini pia aliwaahidi kutafuta uwezekano wa kutengeneza barabara ya moja kwa moja itakayounganisha kata za Mishamo na Katuma yatakapokuwa makao makuu ya wilaya mpya ya Tanganyika.
Waziri Mkuu aliwataka wawe mabalozi wa dhati wa kuelezea umuhimu wa amani nchini kwani wao wamepitia mikikimikiki mingi na wanatambua thamani ya amani.
Mapema, akisoma risala kwa niaba ya wakazi wa Mishamo, Diwani wa kata ya Irangu, Bw. Agustino Mathew alisema wanaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuhitimishwa kwa maisha yao ya ukimbizi yaliyodumu kwa miaka 43.
“Leo ni siku ya pekee kwetu kwa sababu tunafurahia kuhitimishwa kwa maisha ya ukimbizi yaliyodumu kwa miaka 43,” alisema diwani huyo.
Alisema makazi hayo yana wakazi 52,594 ambao wamepatiwa vyeti vya uraia wa Tanzania kati ya 53,379 walioomba uraia. Alisema wakazi 710 walikataliwa maombi yao na 75 walikubalia kurejea Burundi. “Kutokana na mambo mazuri ambayo Serikali ya Tanzania imeyafanya kwetu, tutatii kanuni na sheria za nchi, tutailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutajenga uchumi wa nchi pamoja na kuilinda amani ya nchi yetu Tanzania.”
Alisema wanamshukuru Rais Jakaya Kikwete kutokana na uamuzi wake wa kihistoria wa kuwafanya wao raia wa Tanzania, jambo ambalo limesaidia kuwapa mwelekeo wa maisha yao. “Tunamuomba Mwenyezi Mungu ambariki na kumjalia afya njema na maisha marefu,” alisema.
Hata hivyo, Bw. Mathew alizitaja changamoto zinazowakabili wakazi wanaoishi kwenye makazi hayo na kuiomba Serikali izitafutie ufumbuzi kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema moja ya changamoto ni kutorasmishwa kwa eneo la makazi hayo ambapo aliiomba Serikali iharakishe mchakato wa kubadili hadhi ya makazi yao kutoka kuwa makazi ya wakimbizi na kuwa maeneo yanayoendeshwa chini ya Serikali za Mitaa kama yalivyo maeneo mengine nchini ili waweze kupata huduma za kijamii kwa haraka zaidi.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa huduma za afya, maji, miundombinu, elimu na ukosefu wa umeme ambavyo alisema zinahitaji kuboreshwa ili ziendane na wingi wa wakazi waliopo kwenye eneo hilo.
Kuhusu huduma za kiuchumi, wakazi hao waliomba kupatiwa huduma za kibenki pamoja kuanzishiwa mazao mbadala ya biashara kwani sasa hivi wanategemea zao moja tu la tumbaku. Alisema wakitaka huduma za benki, inabidi waende Mpanda (umbali wa km. 150) au waende Kasulu mkoani Kigoma (umbali wa km. 120).
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni