.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 30 Oktoba 2015

TUME YA HAKI ZA BINAADAMU NA UTAWALA BORA YATOA USHAURI KWA ZEC

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom Nyanduga akiongea na waandishi wa habari (hawako pichani) leo mchana makao makuu ya ofisi za Tume, mtaa wa Barack Obama jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Nyanduga akitoa tamko kuhusu ushauri wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.


TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
Oktoba 29, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
                                
Tamko kuhusu ushauri wa  Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar

1.    Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inapenda kueleza kuwa imepokea tangazo la Mhe. Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), alilolitoa jana tarehe 28 Oktoba 2015 kupitia vyombo vya habari, kuhusu kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2015, na kuahirisha mchakato mzima wa uchaguzi hadi hapo taarifa itakapotolewa tena.

2.    Tume (THBUB) imepitia tamko la Mwenyekiti Jecha kwa makini na kulifanyia uchambuzi kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

3.    Kwa kuzingatia mamlaka ya Tume (THBUB) yatokanayo na katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, hususani;
(a)   Ibara ya 130(1)(a),(c), na (g) vya Katiba (1977), na

(b)   kifungu Na.6 cha Sheria ya Tume (THBUB) na.7/2001 vinavyoipa Tume (THBUB) uwezo wa kisimamia, kuchunguza na kushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora, na; 

(c)   baada ya kuzingatia Ibara za 119 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Sheria na 11 ya 1984, zinoeleza majukumu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC);



4.    Ushauri
Baada ya kupitia Ibara na vifungu mbali mbali vya Katiba zote mbili na sheria husika, Tume (THBUB) imejiridhisha kwamba ina uwezo wa kuishauri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuhusiana na masuala kadhaa yaliyojitokeza katika Tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume (THBUB) imetoa ushauri ufuatao kwa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC):
(i)       Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977,  na Ibara 21 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984[1] zikisomwa pamoja,  zinatoa uhuru wa kila raia kushiriki katika shughuli za uongozi wa Serikali kwa kupitia uwakilishi wa kuchaguliwa na kuchagua kwa uhuru na haki.

(ii)     Kifungu cha 42(6) cha Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar[2] kinaipa Tume (ZEC) mamlaka ya kushughulikia matatizo ya uchaguzi na kuyapatia ufumbuzi kwa utaratibu ulioanishwa katika kifungu hicho.

(iii)    Kifungu hiki kinabainisha mamlaka ya Tume (ZEC) kutangaza matokeo ndani ya siku tatu na endapo kuna matatizo yamejitokeza katika mchakato wa uchaguzi, Tume (ZEC) inatakiwa kuyatafutia ufumbuzi, na baada ya hapo matokeo yatatangazwa ndani ya siku tatu.

(iv)    Tume (THBUB) imepitia sababu zilizotolewa na Mwenyekiti Jecha na kubaini kwamba mambo yote yaliyotajwa yanaweza kutatuliwa iwapo Makamishna wa ZEC wataweka tofauti zao pembeni, na wakafanya kazi kwa pamoja kwa nia njema.

(v)     Tume (THBUB) inashauri kwamba tofauti ama kasoro za kiutendaji zilizotajwa zinaweza kutatuliwa kwa kuhakiki waliopiga kura kwa mujibu wa daftari, na kwa kuzingatia sheria zilizopo.

(vi)    Tume (THBUB) inapenda kumshauri Mwenyekiti wa ZEC kutafakari upya uamuzi wake wa kufuta uchaguzi na matokeo yake yote.

5.    Hitimisho
Mwisho kabisa Tume (THBUB) inapenda kusisitiza umuhimu wa kila mdau wa uchaguzi kuzingata sheria, katika mchakato mzima, kwani bila kufanya hivyo misingi ya utawala bora itakuwa imevunjwa, na hivyo inaweza kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu.

Tume (THBUB) iko tayari kushirikiana na ZEC kuchunguza tuhuma zote zilizotajwa na Mwenyekiti Jecha na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka ili kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Imetolewa na:

(SIGNED)

Bahame Tom Nyanduga
                                                                                       Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Oktoba 29, 2015

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni