.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 11 Novemba 2015

BALOZI SEIF ATEMBELEA JUMBA LA MAKUMBUSHO YA TAIFA ZANZIBAR KUANGALIA UHARIBIFU ULIOFANYIKA KUFUATIA KUANGUKA KWA PAA LAKE



                                                                                          Picha na – OMPR – ZNZ.

Upepo mkali uliovuma ghafla jana mchana umesababisha kuporomoka kwa paa upande wa Magharibi la Jumba la Makumbusho ya Taifa Zanzibar { Beit Al – Ajaib } liliopo pembezoni mwa Fukwe ya Bahari ya Hindi Forodhani Mjini Zanzibar.

Mporomko huo wa Paa hilo pia ulizikumba Gari Tatu zilizokuwa zimeegeshwa pembezoni mwa Jumba hilo ambazo mbili kati yake zilipata athari ya michubuko midogo midogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Karani alieleza hayo wakati akitoa ufafanuzi mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika eneo hilo kuangalia hali halisi ya tukio hilo lililoleta mshituko kwa wakaazi pamoja na wapiti njia katika eneo hilo.

Nd. Sarboko alisema upepo unaokuwa ukivuma katika vipindi vya Majira ya Msimu wa Mvua za Vuli tayari umeshawahi kuathiri Jumba hilo mwaka 2013 na kusababisha kuvunjika katika sehemu ya juu nyuma ya jengo hilo la Kihistoria.

Alisema athari hiyo ilitoa fursa kwa Serikali ya Oman kupitia Ubalozi wake Nchini Tanzania kuonyesha nia ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulifanyia matengenezo makubwa Jumba hilo.

“ Matayarisho ya matengenezo makubwa ya jumba la Makumbusho ya Taifa { Beit Al – ajaib } Forodhani yalianza tokea lilipoporomoka mwanzo mwaka 2013 ”. Alisema Nd. Issa Sarboko Makarani.

Alieleza kwamba taratibu za awali ukiwemo ushauri wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa { Unesco } zilichukuliwa ikizingatiwa kwamba Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa Miji iliyobahatika kuwemo ndani ya Urithi wa Kimataifa.

Mkurugenzi huyo wa Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar alifahamisha kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni Serikali ya Oman kutoa Tenda kwa ajili ya kumteua Mkandarasi atakayehusika kulifanyia matengenezo makubwa Jumba hilo.

Alisema matengenezo ya Jumba hilo yatazingatia zaidi umbile lake lile lile lililokuwepo katika ramani yake ya mwanzo tokea lilipojengwa mnamo mwaka 1883 ambayo itaendelea kuwa kiashiria cha nembo ya Mji wa Zanzibar.

“ Jumba hili la ajabu katika kuzingatia masharti ya Unesco ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe kupitia Urithi wa Kimataifa litafanyiwa matengenezo katika umbile lake lile lile la mwanzo ili kuikabisha haiba ya eneo hilo muhimu kwa Historia na Utalii Duniani ”. AlisemaMkurugenzi Sarboko.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea faraja yake kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar katika kusimamia haiba halisi ya eneo hilo.

Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa Miji michache Duniani iliyopata bahati ya kuteuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mtaifa { Unesco } kuwa urithi wa Kimataifa.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni