Habari na Woinde shizza,Arusha
MRATIBU wa programu ya misitu kutoka shirika la hifadhi ya maliasili
na mazingira duniani (WWF) ofisi ya Tanzania ,Isaac Malugu amesema
kuwa, hekta 400,000 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na ukataji miti na kilimo cha kuhamahama na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Alisema kuwa, hali hiyo imechangiwa pia na shughuli za kibinadamu zinazofanywa kila siku ambapo asilimia kubwa ya nishati inayotumika
hapa nchini inatokana na misitu , hivyo elimu zaidi inahitajika kwa
jamii ili kuokoa upotevu huo.
Malugu alisema kuwa,karibu mikoa yote Tanzania imeathirika na upotevu
huo hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa hali ya ukame katika maeneo mengi ,ambapo kwa mikoa ya kusini bado ina rasilimali ya misitu.
Malugu aliongeza kuwa, shirika hilo limeanzisha utafiti wa kuangalia dhamani halisi ya misitu katika kuhakikisha kuwa inaboreshwa ambapo
utafiti huo utaanza rasmi mwezi huu.
Alifafanua kuwa, katika kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa
kuilinda misitu na kuitunza wamewezesha jamii kutambua umuhimu wa
kutunza misitu kwa kutumia nishati nyingine mbadala badala ya ukataji miti huku wakielimishwa umuhimu wa upandaji miti kwa manufaa yao.
"Pia tumeweza kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimbali ya utunzaji wa misitu huku tukiwawezesha kuwekeza katika misitu hiyo ili
wao wenyewe waweze kuwa walinzi wa rasilimali zao na hivyo kuweza
kuokoa upotevu wa misitu unaofanyika kila wakati.’alisema Malugu.
Naye Dokta Sware Semesi kutoka shirika hilo kwa Tanzania,alisema kuwa
,uwekezaji katika misitu bado ni mdogo sana ambapo elimu zaidi
inaendelea kutolewa kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa misitu.
Alisema kuwa, elimu zaidi imekuwa ikitolewa kwa wananchi katika
usimamizi shirikishi wa misitu ili kwa pamoja waweze kushiriki katika
miradi mbalimbali ya misitu na hatimaye kuweza kufaidi matunda
yatokanayo na misitu kupitia mpango shirikishi wa misitu .
Mkurugenzi wa shirika la hifadhi la wanyamapori Afrika(AWF) ,John Salehe alisema kuwa, wadau mbalimbali kwa ujumla wanahitaji kuunganisha nguvu kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii na kwa umoja ili utunzaji wa misitu uweze kuwa endelevu.
Salehe alisema kuwa, changamoto kubwa iliyopo katika sekta ya maliasili ni pamoja na Wizara hiyo kupewa fedha kidogo sana na serikali ambazo hazitoshelezi kuendeleza miradi ya utunzaji wa misitu, hivyo aliitaka serikali kutoa fedha za kutosha kwa wizara hiyo ili kuendeleza na kuboresha miradi zaidi.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni