Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui akiwahutubia viongozi wa Wilaya, Majimbo na Matawi kisiwani Pemba. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Na Khamis Haji , OMKR
Maalim Seif alisema hayo alipokuwa akihutubia katika mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya viongozi wa Wilaya, Majimbo na Matawi kisiwani Pemba uliofanyika katika ofisi za uchaguzi za CUF Pemba zilizopo Ngoma Hazingwa, Chakechake.
Alisema wanachofanya viongozi wa CCM hivi sasa ni kuchelewesha muda tu, lakini kwa kuwa wananchi wa Zanzibar wamemchagua yeye kuwa Rais na Dunia nzima inafahamu hilo, hatimaye watamwita wenyewe na kumuapisha kuwa Rais wa Zanzibar.
“Wananchi wa Pemba kuleni mshibe, laleni bila ya hofu na tembeeni kifua mbele, hawana njia lazima watakubali maamuzi ya wananchi wa Zanzibar walionichagua niwe Rais wao”, alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema jambo la muhimu kwa wananchi wa Pemba na Wazanzibari wote wasikubali kuchokozeka baada ya hali iliyojitokeza, kwa sababu kuna watu lazima watafanya vitimbi kwa tama ya kuvuruga amani ya nchi.
Alieleza kuwa Chama cha Wananchi CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi tayari kimeamua kwamba hakuna suala la uchaguzi wa Zanzibar kurejewa kwa sababu wananchi wameshafanya maamuzi ya kidemokrasia katika uchaguzi uliokuwa wa huru na haki.
Alisema hakuna haja ya kupoteza muda na kuendeleza propaganda zisizokuwa na msingi kinachopaswa kufanyika hivi sasa ni Tume ya Uchaguzi Zanzibar kumalizia kazi yake na kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25.
“Wache wapoteze muda wataniapisha tu, na wajue muda wangu wa Urais utaanza siku nitakapo apishwa kwa mujibu wa Katiba”, alisema.
Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema jambo linalowatia kiwewe CCM na kutoa visingizio kuhusiana na kura za Pemba ni kutokana na fedha nyingi walizotumia kwa tamaa ya kupata majimbo kadhaa.
Alisema kwamba CCM wamesahau kuwa miaka yote hawapati majimbo kisiwani Pemba na hivyo si ajabu katika uchaguzi wa mwaka huu kukosa viti vyote vya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
Maalim Seif alisema hata huyo mgombea Urais wa Zanzibar kupitia ADC, Hamad Rashid Mohammed ambaye alitegemewa na CCM kupunguza kura za Maalim Seif kisiwani Pemba hakufua dafu na yeye mwenyewe (Hamad Rashid) aliambulia kura 495 tu.
“Viongozi wa CCM maskini walimdanganya sana Dk. Shein kuwa watapata viti Pemba na kura za kutosha za Rais, wametumia fedha nyingi katika uchaguzi huu, lakini walisahau hali halisi ya Pemba na sasa wanahangaika”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.
Alieleza kuwa zipo taarifa kuwa kiasi cha shilingi milioni 70 zilitumiwa na CCM katika jimbo moja tu la Mtambwe, jimbo ambalo katika chaguzi zote zilizofanyika chama hicho hakijawahi kupata kura zaidi ya asilimia tano.
Maalim Seif aliwapongeza mawakala wa CUF katika majimbo yote 54 ya Zanzibar kwa namna walivyo jidhatiti kulinda kura za chama chao na hatimaye kukiwezesha kupata ushindi mkubwa ambao haujapata kutokea Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazuri alisema uchaguzi mkuu uliofanyika kisiwani Pemba mwaka huu ni mfano mzuri wa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki katika nchi nzima.
Alisema kuwa wale wanaodai kuwa kura zimezidi kisiwani humo ni waongo wanaotapa tapa kwasababu kuna watu waliojiandikishwa zaidi ya 200, 000 hawakupiga kura na waliojitokeza kwenda kupiga kura ni 119,000.
Mazrui alisema CCM wamepatwa na maumivu makubwa kisiwani Pemba kutokana na matumizi makubwa ya fedha waliyoyafanya kwa tamaa ya kupata majimbo manne, lakini wananchi wa Pemba hawakuona sababu ya kukichagua chama hicho.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni