Washindi wa tuzo mpya ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya
Kiafrika walitangazwa leo (Novemba 17, 2015). Lengo kuu la tuzo hii ni kutambua
uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha za
Kiafrika kwa lugha nyingine, baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na
pia kwa lugha za Kiafrika.
Washindi wa kwanza wa tuzo hii ni:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya - $5,000: Anna Samwel Manyanza
kwa Penzi la Damu
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi - $5,000: Mohammed K. Ghassani
kwa N'na Kwetu
Zawadi ya Pili katika utanzu wowote - $3,000: Enock Maregesi
kwa Kolonia Santita (riwaya)
Zawadi ya Tatu katika utanzu wowote, $2,000: Christopher
Bundala Budebah kwa Kifaurongo (ushairi)
Hiyo ni miongoni mwa miswada 65 iliyowasilishwa, na kusomwa na waamuzi 6:
Riwaya - Dk. Farouk Topan, Prof. Sheila Ryanga na Prof.
Mohamed Bakari.
Ushairi - Bi. Rukiya Harith Swaleh, Prof. Clara Momanyi na
Prof. Alamin Mazrui.
Waamuzi walisema kuwa, “ Wakitumia lugha inayovutia na iliyo
muwafaka, na mara nyingine lugha cheshi, washindi walizungumzia maswala
yanayozikumba jamii za Afrika Mashariki, kama vile utumiaji wa mihadharati na
athari zake duniani; swala la jinsia – wanawake na haki zao; na ufisadi wa
kisiasa. Huu ni ukweli halisi wa Afrika katika lugha ya Kiafrika.”
Washindi watakabidhiwa zawadi zao katika Tamasha la Fasihi
la Kwani? (Kwani? Lit Fest) litakalofanyika Desemba 3, 2015 katika Klabu ya
Capital mjini Nairobi, Kenya.
Sarit
Shah, Mkurugenzi wa Mabati Rolling Mills Kenya alisema, “Kuongezeka kwa
matumizi ya Kiswahili kuwa ni lugha kuu ya mawasiliano Afrika Mashariki
hakuwezi kupuuzwa. Tunaamini kuwa lugha na tamaduni huboresha mahusiano ya
kikazi na ya kibinafsi. Hapa Safal, hasa hapa Mabati, tunajivunia kuwa katika
jamii hii inayoendelea kukua.”
Abdilatif
Abdalla, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, alisema, “Jambo la kufurahisha ni
kwamba sehemu kubwa ya miswada iliyopokewa ilikuwa ni ya kiwango cha juu. Kwa
sababu ya kanuni za tuzo hii, ni washiriki wane tu ndio wanaoweza kutunukiwa
zawadi. Hata hivyo, ni matumaini yangu kwamba hao washiriki wengine
hawatavunjika moyo, bali wataendelea kushiriki katika mashindano yafuatayo, na
kwamba baadhi yao watafarijika kwa maandishi yao kuchapishwa vitabu pia.
Yanastahili.
Mukoma Wa Ngugi, mwanzilishi-mwenzi wa tuzo hii alisema,
“Kiwango cha msaada tuliopokea kinadhihirisha kuwa kuna uhitaji, na pia uwanja
mpana, wa kuandika kwa lugha za Kiafrika; na kuwa utamaduni wa Kiafrika wa
fasihi unaweza kustawi katika lugha za Kiafrika, na kwamba lugha za Kiafrika
zinaweza kukuzwa kupitia ufadhili kutoka Afrika kwenyewe.”
Lizzy Attree, mwanzilishi-mwenzi mwengine wa tuzo hii
alisema, “Tunawashukuru wote walioleta miswada yao katika shindano hili, na
tunatarajia kuwa tuzo ya mwaka huu itawahimiza waandishi zaidi kushiriki katika
shindano la mwaka ujao.”
Masharti
ya Tuzo:
1.Tuzo itatolewa kwa muswada bora ambao bado haujachapishwa,
au kwa kitabu kilichochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa tuzo, katika
tanzu za riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu, na riwaya za michoro. Jumla ya
dola za Marekani 15,000 zitatolewa zawadi kama ifuatavyo:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya - $5,000
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi - $5,000
Zawadi ya Pili katika utanzu wowote - $3,000
Zawadi ya Tatu katika utanzu wowote - $2,000
2. Kitabu au muswada utakaoshinda utachapishwa kwa Kiswahili
na shirika la uchapishaji la East African Educational Publishers; na diwani bora ya mashairi itatafsiriwa
na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
3. Sherehe ya kuwatuza washindi wanne, itakayohudhuriwa na
washindi wenyewe, itakuwa Kenya. Washindi hao wataalikwa Chuo Kikuu cha
Cornell, watakakokuwa kwa wiki moja; kisha wiki moja nyingine watakuwa katika
asasi shiriki (ya Marekani ama Afrika) mwaka 2016.
Shindano
la mwaka 2016:
Washiriki wanaombwa kupeleka miswada ambayo haijachapishwa,
au vitabu (riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu, au riwaya za michoro),
vilivyochapishwa kwa Kiswahili miaka miwili kabla ya mwaka wa tuzo, kwa: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya Machi 31, 2016. Miswada ya maandishi
ya nathari isipungue maneno 50,000; na ya ushairi isipungue kurasa 60.
Waamuzi:
Waamuzi watabadilishwa kila mwaka na kuchaguliwa na
wadhamini wa Tuzo.
Tarehe
Muhimu:
Tarehe ya mwisho ya kupeleka miswada au vitabu ni Machi 31,
2016. Orodha ya kwanza itatolewa Julai 2016, na washindi watatangazwa Oktoba
2016.
Kwa
Wahariri:
Tuzo
ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Kiafrika ilianzishwa
na Prof. Mukoma Wa Ngugi na Dk. Lizzy Attree mwaka wa 2014 ili kuendeleza
uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha za
Kiafrika kwa lugha nyingine, pia baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa
zenyewe.
Tuzo
ya Mabati-Cornell:
Kwa kiasi kikubwa, tuzo hii inadhaminiwa na Mabati Rolling
Mills of Kenya (sehemu ya Kampuni ya Safal), Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala
ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Masomo na Utafiti ya
Afrikana
Mabati
Rolling Mills:
Mabati ni sehemu ya Kampuni ya Safal, inayotengeneza mabati
katika nchi 11 za Mashariki ya Afrika na Kusini mwa Afrika.
Ofisi
ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu
cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha
shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na
vituo ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za
kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii itaisaidia Halmashauri mpya ya
Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu.
Idara
ya Masomo na Utafiti ya Afrikana ni
Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana,
mazingira ya kielimu, ya kitamaduni na ya kijamii kwenye Chuo Kikuu cha
Cornell, Ithaca.
Tovuti: http://www.asrc.cornell.edu
East African Educational Publisher
(EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi
kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha
kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya
kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana
na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia.
Africa Poetry Book Fund inaimarisha
na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake,
mashindano, warsha na semina pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha,
mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano na vikundi vingine vinavyohusika na
ushairi Afrika.
Tovuti:
http://africanpoetrybf.unl.edu/
Bodi
ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy
Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole
Boyce Davies, Rajeev Shah, Ngugi Wa Thiong’o – na wengine watakaotangazwa
baadaye.
Twitter: @KiswahiliPrize
Kwa
Mawasiliano:
Prof. Mukoma Wa Ngugi, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni