Pichani juu na chini ni baadhi ya viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) wilayani Lolilondo wakisoma na kujadili azimio la pamoja la kumlinda mtoto wa kike kabla ya kulipitisha na kusaini wakati wa kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Katibu wa Baraza la Mila (W) Ngorongoro, Laanoi Munge akisoma azimio la kumlinda mtoto wake baada ya kulifanyia marekebisho ya pamoja mbele ya viongozi wa mila wa wilaya ya Ngorongoro.
Katibu wa Baraza la Mila wilayani Ngorongoro, Laanoi Munge (kushoto aliyesimama) akimsomea baadhi ya maboresho ya vipengele vilivyomo ndani ya azimio hilo Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman (kulia).
Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel akiwasilisha maboresho ya azimio hilo baada ya kulijadili kabla ya kusaini.
Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman akifafanua jambo kwa viongozi hao baada ya kuridhishwa na maboresho ya azimio hilo katika kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha. Kutoka kushoto ni Mkalimani wa kwenye kongamano hilo Mchungaji, Mark Murenga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai pamoja na Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka redio ya jamii Loliondo FM nao walikuwepo kuhudhuria tukio hilo la utiaji saini wa azimio la kumlinda mtoto wa kike.
Baadhi ya maafisa wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na waandishi wa habari waliokuwepo ukumbini kushuhudia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai (kushoto), Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu (wa pili kushoto) Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel (wa pili kulia) pamoja na Ngaigwanan wa Malambo, Miriam Lembirika wakisaini kwa niaba ya viongozi wengine wa mila wa Wilaya ya Ngorongoro, Azimio la Liliondo.Wanaoshuhudia (waliosimama) ni KatibuTawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo (kulia), Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo (wa pili kulia), Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari vya kijamii na Mkufunzi kutoka UNESCO, Rose Haji Mwalimu (wa tatu kulia) pamoja na Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI wa UNESCO, Mathias Herman.
Walioshuhudia tukio hilo wakipiga makofi baada ya zoezi hilo.
Baadhi ya viongozi wa kimila na waandishi wa habari wakishuhudia tukio hilo la kusainiwa kwa azimio la kumlinda mtoto wa kike.
Zoezi la utiaji saini likiendelea kwa kila kiongozi aliyeshiriki kongamano kubwa la siku mbili lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo limefanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha.
Picha ya pamoja baada ya zeozi kukamilika.
Na Modewji blog team
VIONGOZI
wa kimila wa jamii ya Kimaasai na wanawake mashahuri wamepitisha Azimio
la Loliondo lenye lengo la kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha
maendeleo yake kiafya, kielimu na kitamaduni.
Azimio hilo ambalo
limetiwa saini na viongozi hao mwishoni mwa kongamano kubwa la siku
mbili lililofanyika, katika ofisi za halmashauri wilayani Ngorongoro,
linapinga mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike. Mila na
desturi ambazo zimepitwa na wakati.
Kabla ya kupitishwa na
kusaini maazimio hayo viongozi hao wa kimila na mashuhuri walipatiwa
mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuendeleza mijadala na uelewa na hatimae
kuamini kwamba baadhi ya mila na desturi zinachangia na kuchochea
athari za kiafya na kijamii hasa kwa watoto wa kike na kina mama.
Viongozi
hao wamepitisha azimio hilo baada ya kupitia kifungu hadi kifungu na
kuridhia yaliyomo kwa kuzingatia wajibu wao ndani ya jamii na uwezo
mkubwa wa ushawishi kama viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na
akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) .
Aidha walisema kwamba
watatumia nafasi zao kuelimisha jamii juu ya malezi bora ikiwa ni pamoja
na mahali salama pa kulala watoto wa kike na kiume na kuelimisha jamii
umuhimu wa elimu kwa kuwapeleka shuleni hasa kwa watoto wa kike.
“Naomba
viongozi wenzangu twende tukaelimishe jamii juu ya madhara ya tohara
kama tulivyoazimia na kuanzisha mchakato utakaosaidia kupunguza au
kumaliza kabisa matendo ya tohara ndani ya jamii yetu,” alisema
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph
Oletiripai.
Viongozi
hao pia wamesema ni vyema jamii ya kifugaji kuacha kuendelea na vitendo
vya kuwaoza watoto wa kike wakiwa bado wadogo na wakati mwingine kwa
kuwakatisha masomo na kuwalazimisha kuolewa.
“Sisi kama viongozi
tusiendelee kuwa chanzo cha kuendeleza matukio haya kwani ni ya ukatili
kwa watoto wetu wa kike na tutumie nafasi hii kwenda kuwaelimisha
viongozi wenzetu wengine mashuhuri ili kusambaza ujumbe na jamii ijue
athari zinazotokana na ukeketaji pamoja na kuozesha watoto wetu wakiwa
katika umri mdogo,” alisema Laanoi Munge.
Viongozi hao pia
wamedhihirisha kuwa matukio ya vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni
vimechangia utoro nyumbani na kwenda kuishi kwa muda kwenye vituo maalum
kwa kuogopa kufanyiwa tohara.
Watoto hao wamekuwa na hali ya
kutoroka baada ya kugundua kwamba kuna matukio ya ulemavu na athari
nyinginezo za kiafya zinazotokana na ukeketaji na salama yao ni kujitoa
katika jamii hiyo na kutafuta hifadhi kwingine.
Azimio
hilo la Loliondo ambalo pia lilitiwa saini na waganga wa tiba asilia
limetoa mwelekeo wa kuboresha afya ya uzazi, elimu na malezi kwa watoto
wa kike katika jamii ya Kimaasai.
Aidha limetoa namna bora ya
utekelezaji na kupitisha taratibu zitakazosaidia watoto wa kike
wanaokimbia tishio la ukeketaji na kuhakikisha kwamba watasoma na kupata
huduma zote za afya.
Katika maeneo yao baada ya kutia saini
viongozi hao wameahidi kuonyesha ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa
serikali katika ngazi zote, viongozi wa dini, vyombo vya habari, walimu,
wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo katika maeneo yote ndani ya
wilaya ili kuboresha afya ya uzazi, elimu na malezi bora kwa watoto.
Pamoja
utiaji saini wa Azimio la Loliondo,viongozi hao wameliomba shirika la
UNESCO na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kushirikisha viongozi
wengi zaidi, kuendelea kutoa elimu kwa viongozi wa kimila na kuendelea
kuwasaidia katika majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu na
kuwasaidia uratibu wa shughuli zote za kupingana na unyanyasaji na
ukatili wa kijinsia.
Kongamano
hilo lililozaa Azimio la Loliondo ni mwendelezo wa warsha zinazotolewa
na UNESCO kwa ajili ya kutoa elimu ya kuwajengea uwezo na kugawa
majukumu kwa viongozi wa kimila, wamama mashuhuri, viongozi wa dini,
wakunga wa jadi pamoja na waandishi wa habari ili kutekeleza vizuri
ufuatiliaji wa afya ya uzazi na malezi bora kwa watoto katika jamii ya
Kimaasai.
Utiaji saini wa Azimio la Loliondo ulishuhudiwa na
Katibu Tawala Wilaya ya Ngorongoro Bw. Lemuel Kileo, maafisa wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) Bw.Herman Mathias na Bi.Rose Haji Mwalimu.
Kongamano
hilo la siku mbili lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya
ya Ngorongoro limeendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana
na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni