Msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) kwa lengo la kurahisisha kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na shirika hilo kuelimisha jamii kuhusu VVU na UKIMWI.Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika Februri 02,2016 na Februari 03,2016..
Fuatilia hapa chini matukio katika picha 32 zilizoletwa na Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,ndugu Kadama Malunde
Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali AGPAHI (Ariel Glaser
Pediatric Aids Healthcare Initiative) linalojihusisha na mapambano dhidi
ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI limetoa msaada wa baiskeli 104 kwa watoa
huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya jamii katika halmashauri nne
za wilaya mkoani Shinyanga.
Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika
jana na leo ambapo Halmashauri zilizopata msaada huo ni Halmashauri ya
Mji Kahama iliyopata baiskeli 25, Halmashauri ya Msalala baiskeli 32,
Halmashauri ya Ushetu 27 na Manispaa ya Shinyanga iliyopata baiskeli
20.
Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli
hizo ,Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI,
Cecilia Yona alisema msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa
ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza
(Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) ambao ni moja ya
wafadhili wa shirika la AGPAHI
“Mfuko huu wa CIFF unafadhili mradi wa
kusaidia kuongeza usajili wa watoto waishio na VVU kupata huduma za tiba
na matunzo, hivyo, lengo la ufadhili wa baiskeli hizi ni kurahisisha
kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na
shirika hili”, alisema Yona.
“Matumaini yetu ni kwamba baiskeli hizi
zitatumika kwa ajili ya kufuatilia wateja waliopotea katika huduma ya
kupata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV’s),kufuatilia watoto
chini miaka miwili, wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka
15 wanaoishi na VVU pamoja na kuisaidia jamii kupata elimu ya VVU na
UKIMWI", aliongeza Yona.
Yona aliwataka watoa huduma wa afya
waliopata baiskeli hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa huku
akiwasisiza juu ya umuhimu wa kufuatilia wateja waliopotea kwani taifa
linapoteza nguvu kazi kutokana na baadhi ya watu waliopata maambukizi ya
VVU kutozingatia masharti waliyopewa na wataalam wa afya ikiwemo kuacha
kabisa kutumia dawa za ARV’s.
"Bado kuna changamoto ya wateja wetu
kuacha kutumia dawa hasa wanapoona miili yao ina nguvu lakini pindi tu
miili ikianza kudhoofika hukimbilia hospitali,naomba jamii ibadilike,na
kupitia baiskeli hizi mtawafikia wale wote waliopotea katika
huduma",alieleza Yona.
Naye Meneja mradi kutoka AGPAHI mkoa wa
Shinyanga Dkt Gastor Njau alitumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma ya
afya majumbani kuwafikia watoto wenye maambukizi ya VVU kwani bado
watoto wengi hawajafikiwa na kuamini kuwa baiskeli hizo watazitumia
kuwafikia watoto walio wengi zaidi.
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kahama Dkt
Samwel Mwalutambi mbali na kulishukuru shirika hilo kwa kuwajali watoa
huduma ya afya majumbani aliwataka waliopata baiskeli hizo kuzitunza
kama zao huku akiahidi uongozi wa wilaya kusimamia baiskeli hizo katika
vituo vyao vya afya kwa maslahi ya jamii nzima.
Naye Muuguzi mkuu katika Kituo cha afya
Lunguya halmashauri ya Msalala Pili Paulo alisema miongoni mwa
changamoto wanazokabiliana nazo ni wateja wengi kukatisha huduma hali
inayowawia ugumu kuwapata ili warudi katika huduma ya tiba kutokana na
eneo lao kuzungukwa na migodi hivyo watu wanakuja na kuondoka katika
eneo hilo.
Msimamizi wa kituo cha
Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali
ya mji wa Kahama, Dkt John Malulu alisema hivi
sasa hali ya unyanyapaa kwa wagonjwa wa UKIMWI imepungua ukilinganisha
na miaka iliyopita na kilichobaki sasa ni unyanyapaa wa watu binafsi
kuogopa kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU au
la.
Kwa
upande wao baadhi ya watoa huduma ya afya waliopata msaada huo, Stella
Paul na Nobert Zephania walisema kabla ya kupata baiskeli walikuwa
wanalazimika kutumia gharama zao kuwafikia wateja wao hivyo baiskeli
hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuifikia jamii.
AGPAHI ni shirika la kitanzania lisilo la
kiserikali linalojishughulisha na shughuli mbalimbali
ikiwemo kutoa huduma
za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya
UKIMWI,kutoa huduma
ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto,kutoa huduma ya
uchunguzi na huduma za awali ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma za
afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni