Katika kusaidia kupambana na ajali za barabarani kwa watoto wa shule za msingi jijini Dar es Salaam, kampuni ya CFAO Motors Group kwa kushirikiana na Alliance Autos ambao ni wauzaji wa magari ya Volkswagen wametoa msaada wa elimu na vifaa vya usalama barabarani kwa shule 18 zilizo katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.
Akizungumzia msaada huo Meneja wa Volkswagen nchini, Tharaia Ahmed amesema kuwa lengo la kutoa elimu na vifaa hivyo ni kuwasaidia wanafunzi wa shule ambao wengi wao wamekuwa hawana uelewa mzuri kuhusu kuvuka barabara.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni alama za barabarani ambazo zinaonyesha alama za kusimamisha magari ili wanafunzi wavuke, makoti yanayowatambulisha waongozaji, kofia za kuwazuia na jua na mipira ya michezo mashuleni na watatoa elimu katika shule hizo ili kuwasaidia watoto kujua sheria za barabarani.
“Tumeamua kutoa msaada huu kwa shule 18 na tutatoa elimu na tutakabidhi vifaa … tunaamini msaada huu utaweza kuwasaidia watoto hao na tunaamini itasaidia kupunguza ajali barabarani,” alisema Bi. Tharaia.
Akipokea vifaa hiyvo kwa niaba ya Afisa Elimu wa Ilala, Helen Peter alisema wanaishukuru CFAO Motors Group kwa kutambua umuhimu wa elimu na kutoa vifaa vitakavyoweza kusaidia kuongoza wanafunzi wavukapo barabara.
"Tunashukuru sana kwa msaada huu na mmeonyesha ni jinsi gani mnatambua umuhimu wa elimu na sisi tupo pamoja nanyi na tupo tayari kupokea elimu hiyo," alisema Bi. Helen.
Alizitaja baadhi ya shule ambazo zitapata vifaa hivyo kuwa ni Shule ya Msingi Msimbazi, Boma, Mnazi Mmoja, Uhuru Mchanganyiko, Tabata, Ilala, Lumumba, Muhimbili, Buguruni, Kasulu, Mkoani, Msimbazi Mseto, Hekima, Amana, Mtendeni, Buguruni Viziwi na Tabata Jeta na Mtandani.
Pamoja na hayo pia kunataraji kufanyika mashindano ya mbio za magari yaliyo na lengo la kuchangia elimu nchini Rwanda yanayoratibiwa na kampuni ya CFAO Motors Group yanayofanyika nchini na yanataraji kumalizikia nchini Rwanda.
Akizungumzia mashindano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Motors Group, Eric Potin alisema mbio hizo za magari zimeanzishwa na taasisi ya Volkswagen kwa kushirikiana na taasisi ya Opportunity International Germany kwa kutambua kwao umuhimu wa elimu na usalama wa watoto wawapo barabarani.
Alisema kuwa wamekuwa wakisaidia zaidi katika sekta ya elimu na sio mara ya kwanza kufanya mbio hizo za magari kwani mwaka 2013 walifanya mbio kama hizo kutokea Senegal hadi Ghana na mwaka 2015 walifanya kutokea Namibia hadi Malawi na mara zote kampuni ya CFAO Motors Group imekuwa ikihusika kufanikisha mbio hizo.
“Mbio hizi zimeanzishwa na Wajerumani ili kusaidia elimu ya Rwanda na hii sio mara ya kwanza tayari yamefanyika mara mbili barani Afrika na sisi kama CFAO tumekubali kuungana na taasisi ya Opportunity International Germany ili kusaidia upatikanaji wa elimu,” alisema Potin.
Nae Henning Nathow ambaye ndiyo mwanzilishi wa mradi wa go4school ulio na lengo la kusaidia upatikanaji wa elimu bora alisema wanafurahi kufanya mbiao hizo ambazo zina lengo la kusaidia elimu nchini Rwanda wa wanaamini elimu ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia kupambana na umasikini.
Alisema wanataraji kufanya mbio hizo na baada ya kufika Rwanda watayakabidhi magari yanayotumika kwa ofisi za CFAO za Rwanda na baada ya hapo watayauza na mapato yatakayopatikana watayakabidhi kwa serikali ya Rwanda ili kusaidia sekta ya elimu.
“Elimu ni njia ambayo inaweza kusaidia kumaliza janga la umasikini na sisi tuna furaha kufanya mbio hizo kuelekea Rwanda ili kusaidia kupatikana kwa elimu bora Rwanda,” alisema Nathow.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni