Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua gwaride la wahitimu wa mafunzo ya uongozi Mdogo wa Polisi katika ngazi ya Ukoplo, Sajenti na Stafu Sajent hapo chuo cha Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.
Askari wa Kike wa Jeshi la Polisi ngazi ya Ukoplo, Sajenti na Stafu Sajenti wakipita kwa mwendo wa haraka mbele ya mgeni rasmi wakati wakimaliza mafunzo yao ya wiki nane kwenye chuo cha Polisi Ziwani.Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame akitoa maelezo kujiandaa kumkaribisha Balozi Seif kuyafunza rasmi mafunzo ya Uongozi mdogo wa Polisi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Makamanda na wahitimu wa mafunzo ya Uongozi mdogo wa Polisi wakati akiyafunga mafuno hayo.
Balozi Seif akimvisha cheo cha Sajenti Asha Hussein Magungu baada ya kumaliza mafunzo yake na kuwa miongozi mwa askari waliofanya vizuri katika mafunzo yao.
Askari Godrey Kihimba Mjanja akivishwa cheo cha Koplo na Balozi Seif baada kumaliza mafunzo yake na kufanya kufanikiwa kuwa miongoni mwa askari Tisa waliofanya vyema katika mafunzo yao.
Wahitimu wa mafunzo ya Uongozi mdogo wa Polisi ngazi ya Koplo, Sajenti na Stafu Sajenti wakifanya vitu vyao katika kuonyesha moja ya mafunzo waliyoyapata mchezo wa Singe kwenye hafla ya kumaliza mafunzo yao
Wahitimu wa mafunzo ya Uongozi mdogo wa Polisi ngazi ya Koplo, Sajenti na Stafu Sajenti wakicheza ngoma ya utamaduni ya Kilua wakati wa hafla ya kumaliza mafunzo yao hapo chuo cha Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.
Kikundi cha Kwaya cha Wahitimu wa mafunzo ya Uongozi mdogo wa Polisi ngazi ya Koplo, Sajenti na Stafu Sajenti wakitoa burdani ya wimbo maalum kwenye ufungaji wa mafunzo yao hapo Ziwani.
Baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi wakiwemo wale waliomaliza mafuno ya Uongozi mdogo wa Polisi wakimsikiliza Balozi Seif alipokuwa akizungumza nao kwenye ufungaji wa mafunzo hayo. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema askari Polisi yeyote hastahiki kupuuza uhalifu mdogo unaotokea katika eneo lake la kazi ili kuepuka siku moja dharau ya uhalifu kama huo ukaweza kuleta balaa kwa wananchi pamoja na Serikali Kuu.
Alisema kuufumbia macho uhalifu huo mbali ya kuwajengea mazingira mabovu ya kiutendaji askari Polisi hao, lakini pia unaweza kusababisha kuigharimu Serikali kuu kutumia fedha nyingi kuondosha uoza huo, fedha ambazo zinaweza kuelekezwa katika masuala mengine ya Kijamii na uchumi.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Maafisa na askari wa jeshi la polisi kwenye ufungaji wa mafunzo ya Uongozi mdogo wa jeshi hilo ngazi ya Ukoplo, Sajenti na Stafu Sajent.
Alisema hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la upuuzwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya Wananchi mbele ya macho ya Polisi hasa katika uharibifu wa mali za Serikali Mijini na Vijijini.
Balozi Seif aliagiza kwamba wakati umefika kwa jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za kisheria kwa kupelekwa Mahakamani wale wote watakaopatikana na hatia ya kuharibu mali za Serikali iwe bara barani, maskulini au mahali popote hapa Nchini.
“ Tukiyafumbia macho makosa kama haya tunayoyaona mbele ya macho yetu kwa kuhisi kama madogo iko siku moja yatakuja kutugharimu sisi sote ”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea mategemeo yake kwamba mafunzo yaliyotolewa kwa askari hao yataleta mageuzi makubwa ya utendaji katika sehemu watakazopangiwa hasa ikizingatiwa kwamba kozi ya Uongozi mdogo inahusisha askari wenye vyeo vya Ukoplo, Sajenti na Stafu Sajent.
Alisema kutokana na umuhimu wao unaopelekea kupatiwa mafunzo ya kutosha kundi hilo ndio kiunganishi kikubwa kati ya viongozi wa juu na askari wadogo wakiwa wao ni wasimamizi wa kila mara wa watendaji wa kazi za Polisi.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Wananchi walio wengi Nchini watategemea mafunzo waliopata askari hao katika ngazi ya Koplo, Sajenti na Stafu Sajent yatawabadilisha na kuwa watendaji wazuri watakaodumisha uadilifu kwa kuchukia na kupiga vita rushwa.
Alieleza kwamba ni vyema kesi zikaendeshwa kwa haraka, haki itaendeka katika kutekeleza majukumu yao, haki za binaadamu zitazingatiwa kwa lengo la kujenga hjeshima ya Serikali na kuleta uhusiano wa karibu baina yao na Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wahitimu wote wa mafunzo hayo ya uongozi mdogo kwa juhudi walizochukuwa wakati wa mafunzo yao zilizotoa matunda yaliyopelekea kufika hatua ya kupandishwa vyeo.
Mapema Mkuu wa chuo cha Polisi Ziwani Msaidizi Kamishna wa Polisi Deujdedit Kaizilege Nsimeki alisema Jumuia ya chuo cha PolisinZiwani imekuwa ikipata ufanisi mkubwa kulingana na mahitaji ya kisasa yanayowawezesha kwenda na mfumo wa mazingira ya Dunia uliopo .
Kamanda Nsimeki alisema hata hivyo zipo changamoto kwa baadhi ya askari wa jeshi hilo zinazowakwaza katika kupambana nazo akizitaja kuwa ni pamoja na mapambano dhidi ya biashara ya Dawa za kulevya, fedha haramu pamoja na wizi unaendelea kufanywa kupitia mtandao wa kisasa wa mawasiliano.
Akizungumzia mafunzo ya Wiki Nne kwa wahitimu hao yalioanza rasmi Tarehe 16 Febuari mwaka huu Mkuu huyo wa Chuo cha Polisi Ziwani alisema askari hao wamefaulu vyema mafunzo yao ya nadharia na vitendo na wako timamu kutekeleza majukumu yao.
Alisema mafunzo waliyopata askari hao kutoka mikoa mbali mbali Nchini Tanzania yametolewa na wakufunzi wao kulingana na maeneo ambayo askari hao watapangiwa kufanya kazi.
Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame akimkaribisha balozi Seif kuzungumza na wahitimu hao alivipongeza vikosi vyote vya ulinzi hapa Nchini kwa kusimamia vyema ulinzi wa Taifa uliopelekea Zanzibar na Tanzania nzima kumaliza uchaguzi katika misingi ya amani na utulivu.
Kamanda Hamdan akitoa nasaha kwa wahitimu hao kuiga mfano wa askari waliowatangulia ni vyema wakaenda kutumia mafunzo waliyoyapata kwa kufanya kazi kwa uadilifu na nidhamu wakirudi kwenye vituo watakavyopangiwa.
Jumla ya Askari 384 katika ngazi ya Ukoplo, Sajenti na Stafu Sajent wamehitimu mafunzo yao yatakayowajengea uwezo mkubwa wa kufanya kazi zao za kulinda raia na mali zao.
Sherehe hizo zilipambwa kwa gwaride rasmi lililoandaliwa na wahitimu hao ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata fursa ya kulikagua na kupokea heshima.
Baadae Balozi Seif alishuhudia kikundi maalum cha askari waliofanya maonyesho maalum ya zoezi la singe, Judo na Karate ambayo ni muhimu kwa askari hao kujua mbinu za kujilinda na namna wanavyoweza kupambana na adui kwenye matokeo ya uhalifu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Piliwa Rais wa Zanzibar
16/4/2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni