Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
|
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
DARAJA
LA KIMATAIFA LA RUSUMO NA KITUO CHA HUDUMA KWA PAMOJA VYAZINDULIWA RASMI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo Aprili 6, 2016 amezindua
daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha
Rusumo.
Zoezi hilo la uzinduzi lililofanywa
na Mhe. Rais Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Paul Kagame wa Rwanda,
limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kutoka nchi zote mbili,
Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.
Daraja la Kimataifa la
Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani ni kiungo muhimu katika Ukanda wa
Kati (Central Corridor) unaounganisha barabara kuu ya Dar es Salaam - Chalinze – Morogoro – Dodoma – Singida –
Nzega – Tinde – Isaka – Lusahunga na Rusumo kupitia Kibingo Nakayonza hadi
Kigali nchini Rwanda. Mtandao huu wa barabara utakuwa kichocheo kikubwa cha
ukuaji wa uchumi kati ya Tanzania na Rwanda.
Akizungumza katika sherehe
za uzinduzi wa mradi huo, Mhe. Dkt. Magufuli aliwahimiza wananchi kutumia fursa
ya uwepo wa Daraja la Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani Rusumo
kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
ujumla.
Aidha Rais Magufuli
amewaasa wananchi kulinda miundombinu dhidi ya wezi wanaodiriki kuiba alama za
barabarani, vyuma vya madaraja na kuharibu taa za barabarani kwa baadhi ya miji.
Ameagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanalinda miundombinu hiyo na
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokamatwa wakifanya uharibifu
huo.
Aidha licha ya mradi huo
kurahisisha usafairishaji wa bidhaa na watu kwa upande wake Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga alieleza faida kadhaa za mradi huo zikiwemo; kuwa ni kiungo muhimu cha
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda kama vile SADC na COMESA, kurahisisha mawasiliano ya
kijamii baina ya watu wa Tanzania na Rwanda, pamoja na kuimarisha uhusiano na
kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili na nyingine za Maziwa Makuu.
Ujenzi wa Daraja la
Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma Pamoja Mpakani Rusumo ni moja ya miradi
inayotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa nchi za Tanzania na
Rwanda kupitia shirika lake la maendeleo la JICA. Mradi huu kwa upande wa
Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika.
Miradi mingine
inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na
ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera
– Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka.
Mwisho.
Imetolewa
na;
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es
Salaam
06
Aprili, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni