WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema vitendo vya dhuluma, ufisadi na jeuri
vinavyofanywa na watoaji na wapokeaji rushwa vinasababisha wananchi kukosa
haki zao na maisha yao kuwa duni, hivyo amewataka wajumbe na Viongozi wa Jumuiya
ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kupiga vita rushwa katika ngazi zote za
utawala kwenye mamlaka zao na kwa nchi.
“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa
ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa,” amewasisitiza
juu ya umuhimu wa msemo kwa sababu kuna dalili kwamba rushwa ni kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo katika ngazi mbalimbali
zikiwemo za halmashauri, serikali kuu na taasisi mbalimbali za umma.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo mchana wakati wa ufunguzi
wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa ALAT uliofanyika mjini Dodoma ambapo amesema
vitendo vya rushwa vinalalamikiwa sana na wananchi, katika maeneo yote,
hususan katika huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali
katika Serikali za Mitaa.
“Kutokana na ukweli huo, wapo wananchi ambao wameanza
kupoteza imani kwa serikali yao kutokana na kuendeleza vitendo vya rushwa
miongoni mwa jamii. Natoa wito kwenu mkiwa wajumbe wa chombo hiki
muhimu kupiga vita vitendo vyote vinavyoashiria rushwa katika ngazi zote za
utawala kwenye mamlaka zenu na kwa nchi yetu,” amesema.
Amesema hata wakati Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli anazindua Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 alibainisha maeneo mbalimbali
ambayo ni kero kwa Wananchi mojawapo ni tatizo la rushwa miongoni mwa
jamii.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuwa wakati wa kampeni
za uchaguzi rais alipata fursa ya kusikiliza malalamiko mengi ya wananchi
ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa serikali za mitaa kutekeleza majukumu
yake na kuwajibika kwao kama katiba, sheria na sera zinavyoelekeza.
Amesema changamoto nyingine aliyoizungumzia
Mheshimiwa Rais ni upotevu wa mapato na kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu,
matumizi mabaya ya fedha na madaraka, ambapo utekelezaji wa baadhi ya
miradi upo chini ya viwango huku kukiwepo na wizi, uzembe katika mamlaka za
serikali za mitaa. hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa fedha.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuna uvujaji mkubwa wa
mapato yanayokusanywa na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mawakala au
hata baadhi ya watumishi wachache wasio waaminifu, ambapo alitumia
fursa hiyo kuwasisitiza usimamizi mzuri wa mapato ya halmashauri na
kuhakikisha yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ambapo imebainika kuwa ni
salama na itasaidia kupunguza kupovu huo.
“Ninatambua kwamba bado zipo changamoto za utaratibu huu
wa kukusanya mapato kwa njia ya elektroniki. Aidha, zipo taarifa kuwa,
baadhi ya watumishi wa halmashauri ndiyo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya
kodi na tozo mbalimbali za halmashauri, hivyo nawakumbusha watendaji wote
kwamba taarifa hizi zikibainika ni za kweli, hatua za kinidhamu
zitachukuliwa.
Ni vyema wahusika waache tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume
na maadili ya utumishi wa umma,” amesema.
Katika hatua nyingine
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyataka mabaraza ya Madiwani yafanye kazi zake kwa
mujibu wa sheria, ambapo amekemea tabia ya baadhi ya watendaji wa halmashauri
kutokutaka kuulizwa chochote na mabaraza hayo kwa kisingizio kwamba wao ni
watalaamu.
Amesema Mabaraza ya Madiwani ndiyo mamlaka ya wananchi
katika kusimamia halmashauri hivyo kuwazuia Madiwani kuhoji chochote hata
pale ambapo wataalam wamekwenda kinyume na maadili ya taaluma na utumishi wa
umma siyo sahihi kiutendaji, hivyo amewataka watendaji hao kuyaachia
Mabaraza hayo yafanye kazi zake na kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wakea Naibu Waziri wa Nchi, Osisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo amesema watahakikisha
wanatoa maelekezo wanazisimamia vizuri halmashauri katika ukusanyaji wa kodi
kwa mfumo wa kielektroniki.
Pia Jafo amempongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa utendaji
wake na kwamba amewathibitishia Watanzania kuwa Rais Dk. John Magufuli
hakukosea katika uteuzi huo na kwammba umakini wake katika kuchapakazi
umeleta tija nchini.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa,
Steven Muhapa akitoa hutuba ya shukurani kwa Waziri Mkuu, amesema maelekezo
na maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu wameyapokea na wataenda
kuyafanyia kazi.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
|
|
||||
Khadija Mussa-Mwandishi wa Habari
Msaidizi wa Waziri Mkuu
|
Ijumaa, 8 Aprili 2016
MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO MAALUMU WA UCHAGUZI WA ALAT MJINI DODOMA
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni