.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 14 Aprili 2016

SERIKALI YADHAMIRIA KUENDELEZA VIWANDA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda kama mkakati wa kukuza uchumi ili nchi iweze kutoka kwene umaskini na kufikia uchumi wa kati.  

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Alhamisi, Aprili 14, 2016) alipofanya mazungumzo na Waziri wa Biashara wa Oman, Dk. Ali Masoud Al Sunaidy ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.

Amesema mbali na kuimarishwa kwa sekta ya viwanda, pia Serikali imelenga kuboresha sekta za nishati, uchukuzi na kilimo ambazo zitawezesha Taifa kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa kati.  

“Sekta ya viwanda ni eneo ambalo tunataka kuliimarisha kwa sababu litatuwezesha kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini jambo ambalo pia litakuza ajira kwa vijana. Hivyo nawakaribisha mje kuwekeza nchini,” amesema.  

Pia Waziri Mkuu amemuhakikishia kuwa serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa kutoka Oman kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Dk. Al Sunaidy amefurahishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kwamba wapo tayari kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo viwanda vya usindikaji, kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa, na mafuta, gesi, na ujenzi wa bandari.

Akitoa ufafanuzi, Waziri huyo alisema: “Oman ina bandari ya Salala ambayo ni moja kati ya bandari bora duniani yenye uwezo wa kupakua makontena 45 kwa saa. Lakini pia tunayo bandari ya Sohar maarufu kwa bidhaa za viwandani ambayo ina uwezo wa kupakua makontena 32 kwa saa,” amesema.

Dk. Al Sunaidy yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu akiwa ameambatana na wafanyabiashara 80 wa Oman kwa mwaliko wa Kiserikali kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema anatambua kuwa Oman imepiga hatua katika teknolojia ya gesi asili ya kimiminika (LNG) hivyo ana imani Tanzania itapata ujuzi kutoka kwao.

Amesema wafanyabiashara hao wana fursa ya kuwekeza kweye ujenzi ujenzi wa viwanda vya mbolea katika mikoa ya Lindi na Mtwara lakini pia wanaweza kuwekeza kwenye bandari za Tanga, Bagamoyo, Kilwa, Lindi na Mtwara ambazo Serikali imepanga kuboresha miundombinu yake.  

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU 
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S. L. P. 3021, 
11410 DAR ES SALAAM 
ALHAMISI, APRILI 14, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni