.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 16 Juni 2016

BALOZI SEIF AAGANA NA BALOZI MDOGO WA CHINA VISIWANI ZANZIBAR, XIE YUNLIANG

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ALI Iddi Kushoto akiagana na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang kulioa anayemaliza muda wake wa utumishi wa Kibalozi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi zawadi ya Mlango Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang anayemaliza muda wake wa kazi Zanzibar hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie akipokea zawadi za Viungo kutokja kwa Balozi Seif ikiwa kama ishara ya kukamilisha utumishi wake kwa mafanikio hapa Zanzibar.
Balozi Seif akifurahia picha mbali mbali zilizomo ndani ya kitabu Maalum alizopewa zawadi na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie. Picha na – OMPR – ZNZ.



Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Gati kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China { China Harbour Engineering Campany Limited } wameanza kazi ya utafiti wa kuchukuwa sampuli za udongo katika eneo linalotarajiwa kujengwa bandari Kuu ya upakizi na ushushaji wa mizigo mikubwa liliopo kwa Mpiga Duri Mjini Zanzibar.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika matayarisho ya kuaga rasmi akikaribia kumaliza muda wake wa utumishi wa Kidiplomasia hapa Zanzibar.

Balozi Xie Yunliang alisema Jamuhuri ya Watu wa China kwa kuzingatia uhusiano wa Kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar Serikali ya Nchi hiyo imeamua kusaidia Ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri ikilenga kuiondolea msongamano Bandari ya Sasa ya Malindi ambayo uhudumiaji wake haukidhi mahitaji ya sasa ya upakizi na upakuaji mizigo katika kiwango halisi cha Kimataifa.

Alisema Wahandisi wa Kampuni inayotaka kujenga Bandari hiyo ambao wapo Zanzibar kufanya kazi hiyo kwa wiki moja sasa wanatarajiwa kuanza harakati za ujenzi wa Bandari hiyo baada ya kumaliza kwa taratibu zilizobakia pamoja na utafiti huo.

Bw. Xie Yunliang alisema makubaliano ya ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri yamefikiwa kwa pamoja kati ya Viongozi Wakuu wa Zanzibar na wa Jamuhuri ya Watu wa China kufuatia ziara za ushirikiano wa mara kwa mara wa pande hizo mbili.

Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba China itaendelea kuunga mkono harakati za Kiuchumi na maendeleo ili kuona Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar unaendelea kuimarika kila siku.

Alielezea matumaini yake kuona kwamba miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Abdulla Mzee ya Mkoani Kisiwani Pemba, utanuzi wa maegesho ya Ndege katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar iliyopata ufadhili wa Nchi hiyo iko katika hatua za mwisho kukamilika kwake.

Akigusia Sekta ya Elimu Balozi Xie Yunliang alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuwajengea uwezo wa kitaaluma Nchini China baadhi ya Wananchi wa Zanzibar kupitia sekta tofauti za maendeleo.

Alisema zaidi ya Wanafunzi Mia 300 wa Zanzibar wakiwemo wafanyakazi wa Taasisi mbali mbali za Umma wamepata mafunzo kwa mujibu wa fani zao katika vyuo mbali mbali Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.

Alisema mpango huo ulikwenda sambamba na fursa zilizotolewa kwa Viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa kupatiwa semina na mafuno ya mafupi nchini humo.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China ameupongeza Uongozi wa Ofisi ya Mapamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya Balozi Seif kwa jitihada uliochukuwa wa kuipa ushirikiano mkubwa Ofisi ya Ubalozi wake Mdogo uliopo hapa Zanzibar .

Alisema majukumu ya Kidiplomasia yaliyopaswa kutekelezwa na Ofisi hiyo yameratibiwa vyema na kupata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wake kutokana na ushirikiano wa karibu wa watendaji wa pande hizo mbili.

Balozi Xie Yunliang alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Balozi Mpya atakayechukuwa nafasi yake atampa kila ushirikiano katika kuona majukumu yaliyobakia utekelezaji wake anayaendeleza kwa ufanisi wa hali ya juu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi wa Uongozi wa Makampuni ya Uwekezaji wa Mindombinu katika Sekta tofauti ya Jamuhuri ya Watu wa China yaliyoichagua Zanzibar kuweka vituo vyao vya kazi umeleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema yapo Maendeleo makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa Majengo Mapya ya Taasisi za Umma, miradi ya michirizi pamoja na viwanja vya michezo ya Watoto iliyosimamiwa na Makampuni ya ujenzi ya China na kuleta haiba njema katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alimshauri Balozi Mdogo wa China anayemaliza utumishi wake kuutumia uzoefu wa uwepo wake Zanzibar kuwa Balozi wa kuyashawishi Makampuni ya Nchi yake kuja kuwekeza miradi yao ya kiuchumi katika Visiwa vya Zanzibar.

Alisema Wawekezaji wa Jamuhuri ya Watu wa China wana fursa nzuri ya kuwekeza katika miradi ya Uvuvi wa Bahari Kuu inayoweza kutoa mchango mkubwa wa ajira hasa kwa Vijana pamoja na ongezeko la pato la Taifa.

Balozi Seif alieleza kwamba Visiwa vya Zanzibar vimezunguukwa na Rasilmali ya Bahari sehemu zote ambayo bado haijatumiwa ipasavyo kwa shughuli za Uvuvi sambamba na ujenzi wa Viwanda vya usindikaji wa Samaki.

Othman Khamis Ame

 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
16/6/2016.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni