Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ambapo alizungumzia juu ya biashara haramu ya binadamu ambayo imekuwa ikiendendeshwa na mtandao wa watu wasiowaaminifu kwa kuwalaghai mabinti wa Kitanzania kwa kuwaahidi kuwapa ajira nje ya nchi.kwenye mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Sehemu ya Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kwa makini mkutano na waandishi wa habari.
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakisikiliza na kunukuu yaliyokuwa yanazungumzwa na Mkuu wa kitengo Bi. Mindi Kasiga (hayupo pichani)
Mkutano na waandishi wa Habari ukiendelea.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki inachukua fursa hii leo kupeleka taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari juu ya tatizo hili ili kutoa uelewa na kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kukabiliana na changamoto wanazopata Watanzania nje ya nchi wakitafuta maslahi ya kiuchumi ambazo zinaviashiria vya biashara haramu ya Binadamu kwa lugha ya kiingereza lijulikanalo kama (human trafficking) linalozidi kuongezeka.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki inachukua fursa hii leo kupeleka taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari juu ya tatizo hili ili kutoa uelewa na kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kukabiliana na changamoto wanazopata Watanzania nje ya nchi wakitafuta maslahi ya kiuchumi ambazo zinaviashiria vya biashara haramu ya Binadamu kwa lugha ya kiingereza lijulikanalo kama (human trafficking) linalozidi kuongezeka.
Ndugu Wanahabari, Miezi ya hivi karibuni hususan kati ya Mwezi Machi - Mei 2016, Balozi zetu nchini India na Malaysia zimepokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania ambao walipelekwa nchini India, na Thailand kwa ahadi za kupatiwa ajira.Ahadi hizo za ajira zimekuwa zikitolewa na watu wasio waaminifu ambao wanashukiwa kujihusisha na mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu ‘human trafficking’.
Mtandao huo unahusisha raia wa Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na raia wa kigeni waliopo kwenye nchi hizo.Mtandao huo unachofanya ni pamoja na kuwatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18 na 24 na hata chini ya umri huo na kuwalaghai kuwa kuna fursa za ajira katika mahoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani nchi za nje na kwamba watawasaidia wasichana hao kupata kazi hizo pamoja na kuwawezesha kupata VISA na tiketi ya ndege kwa ajili ya kusafiri kwenda kwenye nchi husika.
Wengi wa watu wanaokumbana na ahadi hizo, wanavutika kirahisi kwani wanaona hiyo ni fursa ya kujipatia ajira na kipato cha uhakika. Kwa taarifa tulizozipata kuhusiana na mtandao huo ni kwamba wengi wa Watanzania wanoenda India, huwa wanajua mapema ukweli kuhusu kazi wanayoenda kuifanya huko, ila ugumu wa maisha hupelekea kurubuniwa na kuingia kwenye matatizo makubwa. Nchini India peke yake kuna Watanzania takriban mia tano, wengi wao wakiwa kwenye New Delhi (350), Bangalore (45), Mumbai (20) na wengine wanaelekea Goa.
Ndugu Wanahabari, Kwa upande wa Mashariki ya Kati vilevile kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wa kike kurubuniwa kwa kutafutiwa fursa za kwenda katika nchi za Oman, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu hususan Dubai kufanya kazi za ndani.
Wimbi la Mashariki ya Kati limepata nguvu zaidi kufuatia Indonesia na Philippines kuweka masharti magumu kwa raia wake kwenda kufanya kazi katika nchi hizi hasa kwa kada ya wafanyakazi wa majumbani.Tofauti na nchi za Asia, vijana wa Kitanzania wanaochukuliwa kwenda nchi za Mashariki ya Kati, wengi wao ni wafanyakakazi wa ndani, na wanaondoka wakijua kuwa wanaenda kufanya kazi za ndani.
Wakifika huko, baadhi yao hupata mateso na mikataba yao kukiukwa na hatimaye kuishia mitaani bila msaada.Matatizo yanayowakabili Watanzania nchi za Mashariki ya Kati na Asia. Kulazimishwa kufanya ukahaba na kunyang'anywa Hati za kusafiria ili kuwadhibiti wasitoroke, ndiyo matatizo makubwa zaidi ambayo yamekuwa yakiwakabili Watanzania.
Kufuatia matumaini wanayojengewa na walaghai vijana wa Kitanzania wamejikuta au wamelazimika kukubali kufanya kazi za ukahaba ili kurejesha gharama za kuwasafirisha kutoka Tanzania kwenda katika mataifa hayo ili waweze kurejeshewa Hati zao za Kusafiria pamoja na kupata nauli kwa ajili ya kurudi Tanzania.
Sambamba na matatizo hayo matatizo mengine ni pamoja na Kufanya kazi bila mkataba; Kufanya kazi nyingi ambazo kimsingi zingetakiwa kufanywa na watu wa kada mbili au tatu kufanywa na mtu mmoja; Kufanyishwa kazi tofauti na makubaliano ya awali;
Kulipwa maslahi madogo ikilinganishwa na ugumu wa kazi inayofanywa; Kufanya kazi kwenye familia zaidi ya moja tofauti na makubaliano; Kufanya kazi bila muda maalum na bila kupumzika; Kunyanyanyaswa na kubaguliwa na wakati mwingine kufanyiwa vitendo vya ukatili kama vile kupigwa, kutopewa fursa ya kuwasiliana na mtu yeyote pamoja na kunyanyaswa kijinsia.
Ndugu Wanahabari, Baadhi ya wahanga wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi zetu za Ubalozi kuomba msaada. Balozi zetu zimekuwa zikiwahifadhi Ubalozini na kisha kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani. Baaadhi ya jamaa wamekuwa wakituma tiketi kwa ndugu zao, na mara nyingine maafisa katika Balozi zetu kwa moyo wa kibinadamu wamekuwa wakitoa fedha zao wenyewe kusaidia kununua tiketi za kuwarejesha watanzania waliofanikiwa kuchomoka kwenye mikono ya watesi hao.
Wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka katika Ofisi za Ubalozi za nchi za Asia na Mashariki ya Kati, ili kuweza kuwasaidia wasichana hao kurejea nchini, ambapo kwa hivi karibuni kutoka Ubalozi wa Oman ambapo kulikuwa na wasichana kumi na nane (18), kati yao wasichana kumi (10) wameshasaidiwa kurudi nyumbani na kuunganishwa na familia zao na kutoka ubalozi wa India kulikuwa na wasichana kumi na tano (15) walioleta maombi Ubalozi uwasaidie kwa namna yeyote ile.
Ndugu Wanahabari,Ni wazi kwamba viteno hivyo ni uvunjaji wa sherianna vya kinyama na vinakiuka haki ya binadamu. Ifahamike pia kwamba usafirishaji wa binadamu ni uhalifu kwa mujibu wa makosa ya kupangwa ya Azimio la Umoja wa Mataifa No 55/25 la mwaka 2003 la kuzuia, kukomesha na kuadhibu usafirishaji wa binadamu hasa kwa wanawake na watoto chini ya Itifaki yake.
Pia ni kinyume cha Sheria ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ya Mwaka 2008 yaani <i>“The Anti-Trafficking in Person Act of 2008” Vilevile ni vema ikahafamika kuwa Sheria za nchi wanazopelekwa wasichana hao haziruhusi biashara ya ukahaba na hivyo kupelekea hatari ya kukamatwa na kufungwa ugenini.Ndugu Wanahabari, Hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Baada ya kuona changamoto hizi zinazowakumba Watanzania wanaokwenda kufanya kazi za ndani Nchi za Mashariki ya Kati, Balozi zetu katika ukanda huo ziliaandaa utaratibu maalumu kwa wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuandaa mikataba kulingana na sheria za nchi husika.
Kwa mfano, kwa upande wa Oman tangu mwezi Machi 2011, Ubalozi umeratibu ajira za watanzania 4358 hadi kufikia tarehe 31 Septemba 2015, ambapo kati ya hao 4,033 ni watumishi wa majumbani. Kwa upande wa Mashariki ya Kati, kuanzia Juni, 2015, Serikali iliamua kukataza rasmi Watanzania kwenda kufanya kazi zisizo na ujuzi au za ndani katika nchi hizo hadi utaratibu maalum wa kisheria utakapoandaliwa.
Baada ya katazo hilo, Wizara ikishirikiana na wadau husika iliitisha vikao ili kujadili namna nzuri ya kupata suluhisho la kudumu kuhusu changamoto zinazosababishwa na mtandao huo.Vikao hivyo viliazimia kila Ubalozi katika nchi za Mashariki ya Kati uandae mikataba ya kazi kutokana na muongozo uliokubaliwa na wadau wote. Baada ya kukamilika kwa muongozo huo Serikali ilianza kutoa vibali tena kwa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchi za Mashariki ya Kati.
Vilevile kwa upande wa Asia, kutokana na ushirikiano kutoka kwa Jumuiya za Watanzania waishio katika nchi za Asia pamoja na baadhi ya wahanga wa biashara hiyo katika mataifa hayo, Serikali inashughulikia kupata majina ya wahusika wote wa mtandao huo na kufanya mawasiliano na Serikali za nchi hizo ili kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha katika mkono wa sheria.
Kwa hapa nyumbani, uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na Balozi za nchi ambazo watanzania wetu wanapelekwa ili kubaini watu wote walio sehemu ya mtandao huo hususan wale wanaowezesha upatikanaji wa VISA kwenye Balozi hizo ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria.Vilevile, kupitia kwenu wanahabari, tunatoa wito kwa watanzania wote, tuwe makini pale tunapopata fursa za kazi nje ya nchi.
Kama nilivyosema hapo awali, ni muhimu kujiridhisha kwamba mambo yote ya msingi yanayohusiana na ajira hizo yamekaa sawa ikiwa ni pamoja na:Kuwepo mkataba wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka za Nchi unayotaka kwenda. Kwa hapa nyumbani mamlaka zinazoweza kusaidia ni pamoja na Ofisi za Ubalozi za Nchi husika, Wakala wa Ajira Tanzania - TAESA (Tanzania Bara) au Kamisheni ya Kazi (Zanzibar) Mtanzania asikubali kuanza safari bila kupata mkataba na Kibali kutoka TAESA au Kamisheni ya Kazi.
Wizara inatoa wito kwa Taasisi zote zinazoratibu safari za Nje katika viwanja vya ndege au vituo vya mipakani kuhakikisha hawamruhusu mtu kusafiri nje kwa nia ya kufanya kazi bila kuwa na vibali husika.Kutafuta msaada wa kupata uthibitisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki au Wizara ya Kazi kama kweli kazi uliyoaidiwa ipo- Wizara yetu itaweza kutumia Balozi zetu kuthibitisha.
Na pale unapokwenda Nje, ni muhimu kuhakikisha kwamba unajisajili kweye ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo katika nchi hizo au ubalozi wa Uingereza mahali ambapo hakuna Ubalozi wa Tanzania.
Kutokubali kuweka hati yako ya kusaifiria kama rehani kwasababu yoyote ile; Katika kupata suluhisho la kudumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia Watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi, Wizara kwa kushirikiana na wadau husika inaendelea na jitihada za kusaini Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya Ajira na Kazi baina ya Serikali ya Tanzania na nchi hizo kama ule wa Tanzania na Qatar.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo sio tu kutasaidia kupata fursa za ajira katika nchi hizo bali kutailazimu Serikali ya nchi hizo kushirikiana na Wizara pindi raia wao watapokwenda kinyume na mikataba ya ajira iliyopo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni