Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya
Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Bakari
Nyundo Shime, amesema hatarajii kuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi
katika mchezo dhidi ya vijana Shelisheli utakaopigwa kesho Jumamosi
Julai 2, 2016 kwenye Uwanja wa Stade Linite mjini Victoria.
“Timu haitakuwa na mabadiliko
makubwa. Almost kikosi kitakuwa ni kilekile cha Dar es Salaam kwa
sababu nitampumzisha Job (Dickson Nickson) tu katika mchezo wa kesho,
na nafasi yake atacheza Enrick (Vitalis Nkosi),” amesema Shime leo
Julai 1, 2016 kabla ya kwenda kwenye mazoezi ya mwisho
yatakayofanyika Uwanja wa Linite.
Shime maarufu kwa jina la Mchawi
Mweusi, amesema anauchukulia mchezo huo kwa uzito uleule na kuongeza
ana sababu za kiufundi na kimbinu kumpumzisha Job katika mchezo wa
marudiano kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.
Kwa hali halisi ilivyo timu iko vema
na ikathibitishwa na Shime mwenyewe akisema: “Kikosi kiko vema kwa
maana ya wachezaji wako vizuri na kambi iko vizuri kwa sababu hakuna
majeruhi.” Pia Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija
alithibitisha.
“Sioni kama kuna dalili zozote za
hujuma na kimbinu tumejipanga vema. Tumefuta matokeo ya Dar na tuko
huku tunataka matokeo mapya. Mbinu zangu siku zote ni ushindi wa
nyumbani na ugenini,” amesisitiza.
Serengeti Boys ilitua kwenye Kisiwa
cha Mahe uliko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Visiwa vya Shelisheli
jana Juni 30, 2016 majira ya saa 11 jioni.
Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Ethiopia ilisafiri salama na wachezaji wote 20
wakiwa na viongozi wanane, walikuwa kwenye hali nzuri na kupokewa
vema na wenyeji waliowaandalia usafiri kutoka uwanjani hapo hadi
Victoria- Mji Mkuu wa nchi hii na kufikia Hoteli ya Berjaya Beau
Vallon Resort iliko Kilometa 25 kutoka uwanja wa ndege.
Leo Julai mosi, itakuwa na mazoezi
ya kipindi kimoja tu kwenye uwanja huo kuanzia saa 10.30 jioni (saa
9.30 kwa saa za Tanzania au Afrika Mashariki). Uwanja wa Stad Linite
upo kilometa 10 kutoka hotelini.
Shime ana matumaini makubwa kuiondoa
Shelisheli katika mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao
3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016.
Na ili iweze kufuzu, Serengeti Boys
inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya
aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya
mabao 2-0.
Katika mchezo wa Dar es Salaam
waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah na
Ally Hussein ambaye alifunga kwa penalti na kila mmoja amepania
kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.
Nyota waliosafiri ni pamoja na
makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki
wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick
Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally
Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa,
Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku
washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah
Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima Makame Vitalis.
Serengeti Boys ambayo inahudumiwa na
TFF kwa asilimia 100 ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na
mechi hizo za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya
Shelisheli na Afrika Kusini ambayo itapambana nayo baadaye mwezi
ujao.
Katika kuajindaa na mchezo huo,
Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya
vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth
Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu
katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya
tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
KAMATI YA MAADILI
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajiwa kuwa na kikao chake
Jumamosi Julai 2, 2016 kwenye ukumbi wa ofisi za TFF zilizoko kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, makutano ya barabara za Shaurimoyo na
Uhuru, Ilala jijini Dar es Salaam.
Viongozi watatu kutoka wanachama wa
TFF wanahitajika kufika kwenye kikao hicho kinachotarajiwa kuanza saa
4.30 asubuhi.
Viongozi hao ni Jerry Muro -
Msemaji wa Young Africans S.C
Nassib Mabrouk - Katibu wa MZFA
na Msimamizi msaidizi wa kituo cha Mwanza
Mbasha Matutu - Mjumbe wa
mkutano mkuu Mkoa wa Shinyanga.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni