Kocha Mkuu timu ya Mpira Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa ameita kikosi cha wachezaji 24 watakaoanza kambi ya awali kuajindaa na mchezo dhidi ya Nigeria utakaofanyika Lagos, Septemba 2, 2016.
Kwa mujibu wa Mkwasa, timu hiyo itaingia kambini Agosti 1, 2016 na itadumu kwa siku tano tu kabla ya kuvunjwa na kuitwa tena mwishoni mwa mwezi Agosti, 2016 kujiandaa na kambi ya mwisho na moja kwa moja itakuwa ni kwa ajili ya safari kwenda Nigeria.
Katika kikosi hicho, Mkwasa hajaita nyota wa kimataifa akiwamo Nahodha, Mbwana Samatta wa FC Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa sababu ya majukumu waliyonayo kwenye klabu zao kwa sasa.
Kadhalika, nyota hao wataungana na wenzao nchini Nigeria kwa kuwa mchezo huo upo kwenye kalenda ya CAF na ni wa mashindano. Mchezo huO ambao ni wa kukamilisha ratiba, Mkwasa amesema utakuwa mgumu kwani Nigeria wamebadili benchi la ufundi hivyo kila timu inaungalia mchezo huu kwa jicho la pekee.
Wachezaji walioitwa ni:
Makipa:
Deogratius Munishi
Aishi Manula
Benny Kakolanya
Mebeki:
Kelvin Yondani
Aggrey Morris
Oscar Joshua
Mohamed Husein ‘Tshabalala’
Juma Abdul
Erasto Nyoni
Viungo:
Himid Mao
Mohamed Ibrahim
Shiza Kichuya
Jonas Mkude
Ibrahim Jeba
Mwinyi Kazimoto
Farid Mussa
Juma Mahadhi
Hassan Kabunda
Washambuliaji:
Simon Msuva
Joseph Mahundi
Jamal Mnyate
Ibrahim Ajib
John Bocco
Jeremia Juma
INFANTINO AMSIFU MALINZI
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino amemsifu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwa ni miongoni mwa viongozi wa vyama vya soka duniani walioamua kuendesha soka kwa weledi kutokana na kuratibu mafunzo mbalimbali kwa makocha na waamuzi.
Salamu za Infantino zimetolewa na Msimamizi Mkuu wa kozi ya waamuzi nchini, Carlos Henrique kutoka Afrika Kusini akisema, “Infantino ana ripoti zote ya namna mpira wa miguu unavyoendeshwa duniani. Anasifu Tanzania kwa namna mnavyopiga hatua. Ana ripoti idadi ya makocha walivyokuwa wachache na sasa mna makocha wengine wako kwenye kozi.
“Mbali ya makocha, leo tuko nanyi waamuzi, ni hatua kubwa ambayo Rais Infantino amemsifu Rais wa TFF, Bwana Malinzi,” alisema Henrique.
Henrigue aliyeka waamuzi hao kujikita zaidi kusoma namna sheria 17 za mpira wa miguu zilivyoboreshwa kwa kuondoa zaidi ya maneno 1,000 ili kuja kusimamia vema michezo wa soka huku akiwataka kuwa mahiri wakati wote. Henrique anafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Mark Mzengo kutoka Malawi, Felix Tangawarima wa Zimbabwe na Gladys Onyago kutoka Kenya.
Kozi za Waamuzi wa Mpira wa Miguu wa Tanzania sasa ilianza jana Julai 25, 2016 kwa waamuzi wenye Beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) na waaamuzi waandamizi wanaotarajiwa kuveshwa beji hizo kwa majina yao kupendekezwa FIFA kama watapata matokeo mazuri kwenye kozi inayoendelea.
Kozi ilianza kwa ratiba ya waamuzi wote kuchukuliwa vipimo (physical fitness test) kwa kila mwamuzi chini ya wakufunzi hao kutoka FIFA. Baada ya vipimo, darasa la waamuzi hao litaanza kwa nadharia na vitendo. Darasa hilo litafikia mwisho Julai 29, 2016 kabla ya kuanza darasa la waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) na makamishna wa michezo kwa msimu wa 2016/2017.
SHEIKH SAID BADO MAKAMU MWENYEKITI TPLB
Bwana Said Mohamed bado ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kuingia kwenye wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 2013.
Nafasi hiyo ya Bw. Mohamed ni kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji za TPLB, na aliipata kupitia uchaguzi huo. Pia Makamu Mwenyekiti huyo ni Mwenyekiti wa klabu ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom.
Bw. Mohamed alikuwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Salim Said Bakhresa ambayo pia inamiliki pia timu ya Azam FC kabla ya kustaafu Mei mwaka huu. Licha ya kustaafu ajira yake ndani ya SSB, lakini Bw. Mohamed bado ni Mwenyekiti wa Azam FC.
Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa TPLB pia ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo na wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.
Uchaguzi ujao wa viongozi wa TPLB ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake Hamad Yahya unatarajiwa kufanyika mwakani.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni