Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa Jumanne ya Julai 26, 2016 anatarajia kutangaza kikosi kwa ajili ya kambi ya awali ya wiki moja ikiwa ni maandalizi ya kucheza na Nigeria katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Mkwasa maarufu kama Masters amesema lengo la kambi hiyo itakayoanza Agosti mosi, 2016 ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji kabla ya kuita kambi nyingine rasmi wiki ya mwisho ya Agosti kujindaa na mchezo dhidi ya Super Eagles ya Nigeria unaotarajiwa kuchezwa Lagos Septemba 2, mwaka huu.
“Kikosi change kitakuwa na vijana wengi, mimi ni muumini mkubwa soka la vijana ambao baadhi niko nao na ambao nitawaita, lakini pia mara baada ya ligi kuanza, nitaangalia wengine kabla ya kuwa na program ya ratiba ijayo ya michuano mbalimbali ya kimataifa itakayotolewa na CAF na FIFA,” amesema Mkwasa.
Taifa Stars ilipangwa kundi G kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambazo zitafanyika Gabon, mwaka 2017. Timu nyingine katika kundi hilo ni Nigeria, Chad na Misri ambayo tayari imefuzu baada ya kukusanya pointi 10, Nigeria ina pointi mbili; Taifa Stars ina pointi moja wakati Chad ilijitoa katikati ya mashindano na kukatisha ndoto za Tanzania kucheza fainali hizo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni