.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 25 Agosti 2016

HOTUBA YA MHE. BALOZI AUGUSTINE PHILIP MAHIGA, (MB) WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI WAKATI WA KUMKARIBISHA MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI WAKATI WA UFUNGUZI WA KONGAMAMO LA TATU LA DIASPORA (3RD DIASPORA CONFERENCE) ZANZIBAR, 24 AGOSTI, 2016


Balozi Mahiga

Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Mhe. Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Mhe. Said Hassan Said, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Waheshimiwa Wabunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar;

Waheshimiwa Makatibu Wakuu wa Serikali zote mbili;

Waheshimiwa Mabalozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi;

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Ndugu WanaDiaspora na Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

ASSAALAM ALEYKUM,

Napenda kuchukua nafasi hii na kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwa mwenyeji wetu na kukubali kuwa mgeni rasmi katika kongamano hili la Tatu la Diaspora. Uwepo wako katika Kongamano hili ni ishara kubwa ya mapenzi ya dhati uliyonayo kwa Diaspora na kutambua umuhimu wa mchango wao katika kuleta maendeleo ya nchini.
 

Vilevile, nawashukuru sana waandaji wa Kongamano hili kwa ujumla wao pamoja na wadhamini wetu ambao isingekuwa wao tusingeweza kufanikisha shughuli hii. Shukrani za pekee ziwaendee Kamati ya Mapokezi, kwa mapokezi mazuri tangu tulipowasili hapa visiwani Zanzibar, ninawashukuru sana na kuwapongeza kwa kazi nzuri.

Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapa pole kwa safari ndugu zetu wa Diaspora waliosafiri masafa marefu kutoka kila kona ya dunia kuja kuhudhuria Kongamano hili muhimu. Sina shaka mtafurahia ukarimu wa visiwani na huduma mbalimbali mtakazo zipata katika kipindi chote mtakacho kuwepo hapa Zanzibar. Karibuni sana mjisikie mko nyumbani maana mtu kwao ndio ngao.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilianzisha Idara ya Diaspora mwaka 2010 kwa lengo la kuwatambua Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahamasisha katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutumia mitaji, ujuzi na elimu wanayoipata wakiwa nje ya nchi kwa manufaa ya Taifa lao.

Tangu ilipoanzishwa Idara, kumekuwa na jitihada mahsusi za kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi. Kwa kuanzia, Wizara yangu imekuwa ikiratibu makongamano ya Diaspora ndani na nje ya nchi, na hatimaye Kongamano hili la tatu linalofanyika hapa nchini.

 

Kwa ufupi lengo la makongamano haya ni kutengeneza mazingira wezeshi ya kuwakutanisha Diaspora na Taasisi mbalimbali zilizopo nchini ili kutumia nafasi hiyo kubadilishana mawazo, elimu na ujuzi katika kuleta maendeleo nchini. Azma hiyo pia inalenga kuongeza fursa za uwekezaji na kupanua soko la bidhaa la biashara ndogondogo na za kati ndani na nje ya nchi.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,

Kongamano la Mwaka huu lina kauli mbiu isemayo ‘Bridging Tanzania Tourism and Investment : ’A new Outlook :” kwa kiswahili tunasema kiunganishi cha utalii na uwekezaji: mtizamo mpya ikiwa ni azma ya Serikali kuleta mwonekano mpya wa kujenga Tanzania yenye matumaini ya uchumi wa kati. Diaspora wakiwa wadau wa maendeleo wana nafasi kubwa ya kuimarisha maendeleo ya utalii na sekta ya uwekezaji kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu tukufu ya Tanzania.

Vilevile, Kauli Mbiu hii imechaguliwa ili kuweka msisitizo wa jitihada za Serikali katika kukuza sekta ya utalii na uwekezaji katika uchumi wa nchi, ili kuongeza nafasi za ajira nchini. Tuna imani kuwa Kongamano hili litakuwa ni chachu ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji hapa visiwani kwa kushirikiana na Diaspora wetu katika nchi wanazoishi.
Mhe. Rais,

Ndugu Diaspora,

Nachukua nafasi hii kupongeza ushirikiano na uratibu mzuri baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; kupitia Wizara yangu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Ofisi ya Rais –Zanzibar Ushirikiano huo umezaa matunda mazuri na leo hii tunajivunia uwepo wenu Diaspora ambao ni wa kihistoria. Shukran kubwa zitolewe kwa wadau na taasisi zilizoshiriki kutoa ufadhili ili kulifanikisha Kongamano hili.

Mhe. Rais,
Ndugu Diaspora,

Kongamano hili limeambatana na maonesho ya huduma zinazotolewa na Taasisi mbalimbali kwa ustawi wa jamii ya Diaspora. Maonesho hayo yameshirikisha wafadhili na vikundi vya wafanyabiashara, mashirika ya umma na Taasisi binafsi, pamoja na Diaspora wenyewe.

Aidha, katika siku mbili hizi kutakuwa na uwasilishwaji wa mada zitakazotolewa na Watendaji Wakuu wa Wizara, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi. Lengo ni kuwapatia washiriki, hususan Diaspora ufahamu na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii na uwekezaji ambao unachangia katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ushiriki wa Kongamano hili unajumuisha vikundi vya wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali za utalii, Diaspora waliorejea baada ya kuishi ughaibuni kwa muda mrefu na wadau wengine kutoka taasisi za umma na binafsi ziilizopo nchini.

Vilevile, kama ilivyokuwa mwaka jana, Kongamano la mwaka huu limehudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Lengo la kuwashirikisha maafisa hao ni kuhakikisha kuwa wanafuatilia utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa hapa wakati Kongamano hili. Kwa kutambua kuwa Balozi zetu ndio kiungo muhimu baina ya Serikali na Diaspora.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana.

Mwisho, naomba uniruhusu nichukuwe fursa hii kuipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kufanya kazi hii kwa ushirikiano mkubwa pamoja na kuwashukuru kwa dhati Taasisi zote zilizodhamini Kongamano hili. Ni malengo yetu tutaendelea kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.

Bila shaka Diaspora wamehamasika vya kutosha na kuthibitisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali na iko tayari kuchukua kila hatua kuwashirikisha katika maendeleo chanya ya nchi yetu.

Baada ya kusema hayo naomba nimkaribishe Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili aweze kufungua rasmi Kongamano hili na kuzungumza na Diaspora.

Asanteni kwa kunisikiliza. Karibuni sana Mhe. Rais:

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni