IKIWA inaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbao Fc uliopangwa kuchezwa mwishoni mwa juma hili kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mbeya City fc inataraji kuondoka mjini Shinyanga ijumaa hii kuelekea jijini Mwanza tayari kwa kuikabili timu hiyo iliyopanda daraja kwa ‘mtereko’ tiketi ya mezani.
Mapema leo kwenye uwanja wa Kambarage wakati wa mazoezi ya asubuhi afisa habari wa kikosi hiki, Dismas Ten, amesema kuwa City itaondoka mjini Shinyanga ijumaa jioni kuelekea jijini Mwanza ikiwa na lengo moja tu la kuvuna pointi tatu zingine kwenye uwanja wa CCM Kirumba kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa juma lililopita dhidi ya wenyeji Toto Africans.
“Tumekuwa hapa Shinyanga toka siku ya jumatatu, kwa ajili ya mazoezi na matayarisho ya mchezo wa jumamosi,Mwalimu alichagua kufanya mazoezi Kambarage kwa lengo moja tu la kupata utulivu na kuandaa kikosi vizuri ili kuhakikisha tuanshinda na kupata pointi tatu kwenye siku nzuri ya Septemba 3 , kikosi chetu kiko sawa, pasipo majeruhi yeyote na tunakwenda Mwanza kucheza kwenye uwanja ambao siku zote tumekuwa na bahati nao”. alisema
Akiendelea zaidi Ten aliweka wazi kuwa kiungo Geoffrey Mlawa na mshambuliaji Omary Ramadhani waliyopata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans wamerejea kwenye hali nzuri na anaweza kuwa sehemu ya mchezo huo wa jumamosi endapo Mwalimu Kinnah Phiri atapenda kuwatumia.
“Dakika 90 zilizopita tulizihitimisha kwa kupata majeruhi wawili kwa Omary Ramadhani na Geoffrey Mlawa, jopo la madaktari wamethibitisha kuwa wachezaji hao wako sawa na wanaweza kucheza kwenye mchezo wa jumamosi ingawa jambo hilo litategemea na maamuzi ya mwalimu, kuwepo kwao kikosini kutaongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo ni muhimu kwenye kusaka pointi tatu,hasa ukizingatia kiwango kizuri walichokionyesha kwenye mechi dhidi ya Toto Africans” alimaliza.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni