WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewasili Nairobi, Kenya kuhudhuria Mkutano wa Mkuu wa Sita wa Wakuu
wa Nchi wa TICAD (TICAD VI) utakaofanyika Agosti 27 -28, mwaka huu.
Waziri Mkuu anahudhudia mkutano huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe
Magufuli.
Leo asubuhi (Ijumaa, Agosti 26,
2016) Waziri Mkuu amekutana na viongozi wakuu mbalimbali wa makampuni
ya kibiashara kutoka Japan ambao wamekuja kuhudhuria mkutano huo.
Waziri Mkuu amekutana na Makamu wa
Rais wa Kampuni ya Chiyoda Corporation, Bw. Tadashi Izawa ambapo
katika mazungumzo yao, pamoja na kuangalia fursa nyingine katika
sekta ya gesi Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa mafunzo ya
kujenga uwezo wa wataalamu kwa sekta ya gesi hususan usindikaji wa
gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi (Liquefied Natural Gas).
Bw. Izawa amemweleza Waziri Mkuu
kwamba wamefurahiswa na taarifa za ugunduzi wa gesi ya Helium hapa
nchini Tanzania na kwamba kampuni yake ina teknolojia na uzoefu wa
muda mrefu katika kutekeleza miradi ya gesi (Gas value Chain Planning
and Execution).
“Tunao uzoefu wa muda mrefu, pia
tunazo teknolojia za kuendeleza sekta ya gesi ikiwemo Helium kwa
mfano ujuzi wa kutenganisha gesi asilia na helium (Separation of
Natural Gas and Helium). Tumetekeleza miradi ya namna hii nchini
Qatar ambayo kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa gesi hiyo duniani
ikitanguliwa na Marekani,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yatafanyika
kuanzia mwakani na yatalenga vijana wasiopungua 10 kutoka Tanzania
ambao wamehitimu shahada za uhandisi kwani wameshafanya hivyo kwa
vijana wanane kutoka Msumbiji.
Waziri Mkuu alimshukuru Vw. Izawa
kwa mpango wao wa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania lakini akamtaka
pia waangalie uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaotoka maeneo husika
yenye gesi ili wapatiwe mafunzo ambayo yatawawezesha kumudu baadhi ya
kazi kwenye viwanda vya kusindika gesi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekutana
na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada ya
Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Hiroshi Kato na kujadiliana mambo
kadhaa yakiwemo ya nishati na miundombinu.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Kato
alimweleza Waziri Mkuu nia ya shirika hilo kuendelea kusaidia miradi
mbalimbali ya kilimo hapa nchini na hasa katika sekta za afya, maji,
kilimo na miundombinu ambazo imekuwa ikijihusisha nazo kwa muda mrefu
sasa.
Waziri Mkuu alimshukuru kwa ushiriki
wa shirika hilo kwenye miradi ya nishati ya Kinyerezi na akamtaka
aendelee kuisaidia Serikali ya Tanzania inainginia kwenye awamu ya
tatu ya Kinyerezi (Kinyerezi III).
Katika hatua nyingine, Balozi wa
Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe alimwoba makamu wa Rais hyo
waangalie uwezekano wa kuwekeza kwenye sekta za nishati na
miundombinu ya mkoa Dodoma hasa katika kipindi ambacho Serkali
imeamua kuhamia huko.
“Tunaomba muangalie sana suala la
kuendeleza nishati ya umeme kwani nchi yetu imeamua kuwa nchi ya
viwanda. Tutahitaji kuwa na umeme wa kutosha kuendesha viwanda vya
usindikaji bidhaa zetu, lakini pia si mbaya mkiangalia suala la
kuboresha miundombinu ya barabara na usafirishaji katika mji wa
Dodoma,” amesema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 26, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni