Balozi Mdogo Mpya wa India Bwana Tek Chand Barupal wa kwanza kutoka kushoto akizunghumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea zawadi ya ukumbusho kutoka kwa Mdogo Mpya wa India Bwana Tek Chand Barupal aliyefika ofisini kwake kujitambulisha rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiomba Serikali ya India pamoja na fursa za masomo ya juu inazotoa kwa vijana wa Zanzibar, ikatoa upendeleo maalum wa mafunzo ya uhandisi ili kusaidia kuziba pengo la fani hiyo katika Taasisi za Umma.
Alisema Wahandisi kadhaa wa Zanzibar waliopata mafunzo ya Muda mrefu na kufanyakazi katika idara na Mashirika mengi ya Umma hivi sasa tayari wengi wao wameshastaafu na wengine wako njiani kukamilisha muda wao wa utumishi Serikalini.
Akizungumza na Balozi Mpya wa India Zanzibar Bwana Tek Chand Barupal aliyefika kujitambulisha rasmi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Balozi Seif alisema upungufu huo wa watumishi wa umma wenye fani ya Uhandisi unaweza kuleta msuko msuko endapo hautachukuliwa hatua za haraka.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia baadhi ya Taasisi zake wakati mwengine hulazimika kuendelea kuwatumia wahandisi wenye ujuzi maalum wa muda mrefu licha ya wahandisi hao kufikia muda wao wa kustaafu kitendo ambacho kama hakikuandaliwa mpango maalum wahandisi wapya waliopo nchini wanaweza kukosa uwezo mkubwa wa kushika nafasi hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi Mdogo huyo wa India hapa Zanzibar ameipongeza India kwa jitihada zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya Maendeleo akiitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na huduma za maji safi pamoja na Kiwanda cha Matrekta.
Alimuahidi balozi Tek kwamba Zanzibar pamoja na Tanzania kwa ujumla zitaendelea kuimarisha ushusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili hasa ikizingatiwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Viongozi waasisi pande hizo mbili katika kuuasisi uhusiano huo.
Hata hivyo balozi Seif alimuomba Balozi Tec Chand Barupal kutumia Diplomasia aliyonayo kuendelea kuyashawishi Makampuni na Taasisi za nchi yake kusaidia miradi mengine ya maendeleo kama kilimo cha umwagiliaji maji, Afya pamoja na Viwanda vidogo vidogo Visiwani Zanzibar.
Mapema Balozi Mpya mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana Tel Chand Barupal alisema India katika mpango wake wa kuimarisha uhusiano na Mataifa ya Bara la Afrika imeongeza fursa ya masomo kwa Vijana wa Zanzibar kutoka wanafunzi 60 mwaka 2014/2015 hadi wanafunzi 75 mwaka 2016/2017.
Bwana Tek alisema utiaji saini mikaba mbali mbali umeshafanyika kati ya Viongozi wa India na Tanzania kwenye miradi tofauti ya Maendeleo na uchumi ikiwa na azma ya kuimarisha uhusiano uliopo wa miaka mingi kati ya pande hizo mbili rafiki.
Balozi mdogo Tek Chand alimuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba katika kipindi chake cha utumishi hapa nchini ataongeza ushirikiano na viongozi wa Zanzibar ili kuona kundi kubwa la vijana linajengewa mazingira bora ya kujitegemea kimaisha katika mpango wa Serikali kuu wa kuimarisha mafunzo na miradi ya kazi za amali.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni