Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya
Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya
Iran Balozi Hussein Mollale Abdullahi akizungumza na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Jengo la Baraza la
Wawakilishi lilipo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na –
OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akipokea zawadi kutoka
kwa Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi
za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Hussein Mollale mara
baada ya mazungumzo yao. Wa kwanza kutoka Kulia ni Katibu wa kwanza
Msaidizi wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Mjini Dar es
salaam bwana Mohammad Dehghani.
Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran
imeahidi kuendelea kutoa fursa zaidi ya Mafunzo ya Elimu ya juu kwa
wanafunzi wa Zanzibar katika mpango wake wa kuimarisha uhusiano
uliopo kati yake na Zanzibar uliodumu kwa muda mrefu sasa.
Fursa hizo zitazingatiwa zaidi
katika fani ya Uhandisi kwa vile Visiwa vya Zanzibar tayari viko
katika maandalizi ya utafiti wa mafuta na gesi ikijiandaa kuelekea
katika uimarishaji wa Sekta ya nishati itakayosaidia kubadilisha
uchumi wa Zanzibar katika miaka michache ijayo.
Mkurugenzi Mkuu kutoka Idara ya
Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamuhuri ya Kiislamu ya
Iran Balozi Hussein Mollale Abdullahi alieleza hayo wakati
akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi Ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Balozi Hussein alisema Iran kwa vile
imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zilizopelekea kuongoza nafasi ya
Pili katika uzalishaji wa mafuta na Gesi Duniani imejitolea kuunga
mkono Mataifa Rafiki katika azma ya Mataifa hayo kujenga uwezo zaidi
wa kujitegemea.
Akizungumzia miradi ya kujitegemea
Balozi Hussein alisema Taifa lake lilioko Mashariki ya Kati tarayi
limeshatoa msaada mkubwa wa Vifaa na mashine kwa ajili ya chuo cha
Amali kiliopo Mkokotoni ili kuwajengea uwezo vijana wanaopata mafunzo
ya ujasiri amali kwenye chuo hicho.
Alisema Mafunzo ya Amali
yanayojumuisha fani za ufundi, biashara pamoja na ujasiri amali ndio
njia sahihi ya kumuandaa kijana mara amalizapo masomo yake ili apate
uwezo mkubwa utakaomuwezesha kujitegemea katika kuendesha maisha
yake ya kila siku.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Jamuhuri ya
Kiislamu ya Iran kwa msaada wake mkubwa iliyotowa kwa Chuo cha Amali
Mkokoni msaada ambao utaleta ukombozi mkubwa kwa kundi kubwa la
Vijana kuweza kuwanyooshea njia ya kujitegemea wenyewe binafsi.
Balozi Seif alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuanzisha vyuo vya Amali Unguja na
Pemba lengo likiwa kupunguza wimbi kubwa la ukosefu wa ajira ambalo
Serikali Kuu pekee haina uwezo wa kuajiri vijana wote wanaomaliza
masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliiomba Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Mkurugenzi
Mkuu huyo kutoka Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya
Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Balozi Husseid kuendelea kuisaidia pia
Zanzibar katika Sekta ya Afya.
Balozi Seif alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya tayari imeshaanza
matayarisho wa ujenzi wa Vitengo vya kutibu Maradhi ya Saratani
pamoja na Moyo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mambo ambayo Iran
inaweza kusaidia utaalamu na Madaktari kwa vile imeshapiga hatua
kubwa katika fani hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni